Tanapa yaja na mkakati kudhibiti uvamizi wa tembo

Muktasari:
- Tanapa yajipanga kuondoa tatizo la tembo kuua watu na kuharibu mazao shambani.
Katavi. Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Shirika la hifadhi za taifa Tanzania (Tanapa) Jenerali Mstaafu George Waitara amesema shirika hilo linajipanga kuliondosha tatizo la tembo kuua watu na kuharibu mazao shambani .
Waitara amebainisha hayo alipokuwa akifunga mafunzo ya ajira mpya “Recruit Course” kwa wahitimu 57 Tanapa yaliyofanyika kituo cha Mlele mkaoni Katavi.
Akiwahutubia wahitimu hao amesema maliasili zinahujumiwa na majangili japo kwa sasa tatizo hilo limedhibitiwa kwa kiasi kikubwa hasa kuzuia ujangili wa tembo.
Soma hapa:Mbunge alia tembo kuvamia Mwanga
“Sasa hivi hata huku mnasikia kulalamikiwa kila wakati tembo wapo vijijini, wengine huwa wanasema tembo wameongezeka inashangaza katika kipindi kifupi tembo wanaweza kuzaliana kiasi hicho haiwezekani?,amesema Waitara
Amesema awali tembo walikuwa wametawanyika na kwamba wamerudi kwasababu wana amani na waliosababisha amani hiyo ni jitihada za askari wa Tanapa.
Soma hapa: Tembo wazua kizaazaa vijiji saba Nachingwea
“Hizi changamoto za kuua watu kula mazao tutajua namna ya kuziondosha,tembo ni mnyama mwenye akili sana anapita maeneo aliyopita miaka hamsini iliyopita, binadamu tunaongezeka hatujui tupo kwenye maeneo yao, amerudi anafuata mlemle,rai yangu mnakokwenda endeleeni kuelimisha ,”amesema.
Awali akisoma taarifa ya mafunzo ya askari wa ajira mpya Mhifadhi Mwandamizi Makao makuu Emmanuel Kaaya amesema wahitimu hao wamefanikisha kukamata majangili 19 na gobore tatu katika hifadhi ya Katavi.
“Pia walikamata ng’ombe 440,wachungaji 18,mbwa wawili waliuua,unga wa gobore gm 500 na risasi 42,,shoka 8,baiskeli 7, misumeno ya mbao 2,panga 7,visu 4, nyama pori gm 100 na ya nguruwe kilo 70,’amesema Kaaya .
Ameongeza kuwa sh 46 milioni zimepatikana baada ya watuhumiwa kukamatwa na kupigwa faini akidai kuwa wahitimu waliofanyia mafunzo yao ya vitendo katika hifadhi ya taifa Serengeti wamefanikiwa kutegua nyaya za mitego 239 na kukamata majangili 14.
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo Anderson Anton na Fartuma Hamis waliotunukiwa vyeti kwakufanya vizuri darasani wameeleza mbinu walizozitumia ni kusikiliza kwa umakini walivyokuwa wakifundishwa.
“Tuwashukru wakufunzi wetu wametufundisha vizuri na siyo kwamba tumekuwa bora wawili tu hapana wote tumefanya vizuri lakini ilitakiwa wapatikane wawili,”wamesema.