Tanapa yataja sababu kuchelewa kuzima moto mlima Kilimanjaro

Muktasari:
Tanapa imetaja changamoto katika kuuzima moto mlima Kilimanjaro, huku ikipongeza wananchi walivyosaidia.
Dodoma.Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa sababu zilizochangia kuchelewa kuzima moto katika mlima Kilimanjaro kuwa ni vitendea kazi duni ikiwemo ukosefu wa ndege ya kuzima moto.
Kamishina wa uhifadhi wa Shirika la hifadhi za Taifa (Tanapa) Dk Allan Kijazi ameeleza hayo leo Jumanne Novemba 3, katika ofisi za wizara hiyo Mtumba Jijini Dodoma alipozungumza waandishi wa habari.
Dk Kijazi ambaye ni naibu katibu mkuu wa Wizara ya Maliasi na Utalii, ametaja chanzo cha moto huo kuwa ni kichungi cha sigara kilichowashwa na mmoja wapagazi waliopanda mlima huo na kwamba hatua za kisheria zimechukuliwa dhidi ya watuhumiwa wa kitendo hicho.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, moto huo uliteketeza kilimoita za mraba 95 na kusababisha hasara ambayo tathimini yake bado inafanyika, ili kujua kiasi halisi cha hasara.
Oktoba 11, 2020 moto ulizuka katika mlima Kilimanjaro na ilichukua siku tano kuuzima na pia zikatumika siku zingine 12 kwa ajili ya kuuzima moto kwenye visiki, magogo na mboji zoezi lililokamilika Oktoba 28.
“Tunamshukuru Mungu zoezi hilo halikuzuia shughuli za utalii ambao umeendelea hadi sasa, ingawa hatujajua hasara iliyosababishwa na moto huo. Tunahitaji kuwa na vifaa vya kisasa ikiwemo hata ndege zisizo na rubani ili kuondokana na changamoto iliyotupata,” amesema Dk Kijazi.
Ameeleza changamoto nyingine ni miundombinu, kwani njia zina makorongo makubwa, hivyo inakuwa vigumu maeneo hayo kufikika ikiwemo namna ya kuwapelekea chakula watu waliokuwa wanajitolea kufanya kazi ya kuzima moto.
Pamoja na hayo, ameshukuru watu wanaoishi kuzunguka mlima huo kwamba wamefanya kazi nzuri yenye kustahili pongezi kwa kuwa waliwezesha kuuzima moto huo.