Tanzania haitawatupa wakimbizi - Mkurugenzi

Muktasari:

  • Tanzania yapokea wakimbizi zaidi ya 11,000 katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia mwezi Machi hadi Juni, kutoka DRC, huku kila siku walipokelewa wakimbizi kati ya 29, 30 au zaidi.

Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha siku ya wakimbizi ambayo hufanyika kila ifikapo Juni 20, katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Machi hadi Juni mwaka huu, Tanzania imepokea wakimbizi zaidi ya 11, 000 kutoka nchi ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kwa mujibu wa Mkurugenzi msaidizi anayesimamia kambi na makazi ya wakimbizi katika idara ya huduma kwa wakimbizi Nsato Marijani, katika kipindi hicho kila siku walipokelewa wakimbizi kati ya 29 hadi 30.

Huku idadi hiyo ya wakimbizi zaidi ya 11,000 kutoka nchi moja ni kubwa zaidi kuwahi kutokea nchini ukilinganisha na vipindi vingine.

Marijani ameyasema hayo leo, jijini hapa alipohudhuria mdahalo uliondaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR wakishirikiana na chuo kikuu cha Dar es Salaam wakiangazia utatuzi wa masuala ya wakimbizi.

Maadhimisho hayo ya mwaka huu yana kauli mbiu isemayo “Matumaini mbali na nyumbani”.

Wakati akichangia mada katika mdahalo huo, uliofanyika UDSM, Marijani ameeleza kwamba licha ya kuendelea kupokea wakimbizi changamoto wanayokumbana nayo ni kupungukiwa kwa rasilimali za kuwahudumia wakimbizi hao, rasilimali amabazo huwa wanazipata kutoka jumuiya ya kimataifa.

“Jukumu la kuhudumia wakimbizi linazidi kuielemea serikali ya Tanzania, hatuwezi kuwatupa hawa ni ndugu zetu na hatufanyi haya kwasababu ya mikataba, nchi hii kwa asili yake anapopata shida jirani kama nchi lazima tujitoe kutoa msaada,” amesema

Marijani ameeleza kwamba wanaiomba jumuiya ya kimataifa kuchangia katika suala hilo katika kuhakikisha kwamba wakimbizi wanapata huduma sitahiki, kwani Tanzania imejitolea sana katika hili suala, kwa kutoa ulinzi pamoja na kuwahusisha wakimbizi katika programu mbalimbali za kijamii.

“Hili jambo halijaanza jana limeanza miaka mingi, kwani katika makazi na vijiji mbalimbali maendeleo yapo shule mpya zina jengwa, hospitali kwaajili ya kuhudumia wakimbizi,” amesema.

Naye, Mhadhiri mwandamizi katika idara ya Jiografia kutoka chuoni hapo Opportuna Kweka amesema vyombo vya habari vinapaswa kutoa elimu kwa jamii kuhusu wakimbizi kwani wao ni watu kama walivyo watu wengine.

“Watu wengi wamekuwa wamekuwa wakitambua wakimbizi wengi ni hatari jambo ambalo si kweli,” amesema

Pia amesema miongoni mwa nchi zenye wakimbizi wengi ni zile ambazo zimepata changamoto ya kivita mara kwa mara.

Naye mwakilishi kutoka UNHCR, George Kuchio amesema huwa wanaadhimisha siku ya wakimbizi duniani, ili kuhakikisha wakimbizi wanapata faraja kama ilivyo kwa watu wengine.

“Tunaadhimisha hii siku ili kuwapatia faraja wenzetu, tunataka wasijisikie kuwa ni watu wa kutengwa kwani binadamu wote sisi ni sawa,” amesema

Hata hivyo, takwimu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, zinaonesha kwamba mwishoni mwa mwaka 2022, watu milioni 108.4, walilazimika kuhama katika makazi yao kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo vita, migogoro ya wenyewe kwa wenyewe, pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu.