Tathmini yafanyika dharuba iliyoharibu mitumbwi 212 Ziwa Victoria

Muktasari:
Serikali inaendelea kufanya tathmini kujua hasara iliyotokana na tukio la dhoruba kali lililokumba mialo ya Busekela na Buira Wilaya ya Musoma mkoani Mara na kuharibu mitumbwi 212.
Musoma. Serikali inaendelea kufanya tathmini kujua hasara iliyotokana na tukio la dhoruba kali lililokumba mialo ya Busekela na Buira Wilaya ya Musoma mkoani Mara na kuharibu mitumbwi 212.
Akizungumzia tukio hilo lililotokea Machi 20, 2023, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Halfan Haule amesema tathmini ya awali imebaini kuwa mitumbwi 29 imeharibika kiasi cha kutoweza kutengenezeka huku 183 yaliyosalia yanaweza kukarabatiwa.
Pamoja na kuharibu mitumbwi, dharuba hilo lililoandamana na upepo mkali pia imeharibu nyavu za wavuvi, zikiwemo nyavu 68 za kuvua dagaa.
"Tumekubaliana wamiliki ambao mitumbwi yao inaweza kukarabatiwa waanze kuyafanyia ukarabati ili kuwawezesha kurejea kwenye shughuli zao za kila siku,” amesema Dk Haule
Amesema uongozi wa Serikali Wilaya ya Musoma kwa kushirikiana na Mbunge wa Musoma vijiini, Profesa Sospeter Muhongo inafanya mawasiliano na baadhi ya wadau kutafuta namna ya kuwasaidia wavuvi kukarabati mitumbwi yao.
“Kutokana na hali ngumi ya kiuchumi na hasara iliyotokea, baadhi ya wavuvi hawana uwezo wa kukarabati mitumbwi yao na Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini inatafuta wadau watakaosaidia ukarabati wa mitumbwi yao ikiwemo kutoa msaada wa vifaa vya matengenezo kama mbao, rangi na misumari,” amesema Dk Haule
Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo amesema thamani ya awali inaonyesha kuwa ukarabati wa mtumbwi mmoja unaweza kugharimu zaidi ya Sh1.7 huku Sh1.4 milioni zikihitajika kwa ajili ya matengenezo ya nyavu moja ya kuvua dagaa.
“Hii ni gharama kubwa kwa wavuvi wetu kuweza kumudu; tunawaomba wadau wenye mapenzi mema kujitokeza kuwasaidia kukabiliana na changamoto hii iliyotokana na janga la dharuba,” amesema Profesa Muhongo
Jumanne Bwire, mmoja wa wavuvi katika mwalo wa Busekela ameishukuru Serikali na Ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini kwa kuwa karibu nao tangu siku ya tukio hadi sasa huku akiwaomba wadau wa maendeleo ndani na nje ya Mkoa wa Mara kujitokeza kusaidia wavuvi kukarabati mitumbwi yao na kutengeneza au kununua nyavu mpya ili waweze kurejea kwenye shughuli zao ambazo zimekwama tangu janga hilo litokee.