Tawja: Waathirika udhalilishaji mtandaoni waoga kuripoti
Baadhi ya wanafunzi wa Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini (Makumira), Arusha wakifuatilia mafunzo ya kupinga ukatili wa kijinsia hasa udhalilishaji wa kimtandao leo Ijumaa Desemba Mosi, 2023 jijii Arusha. Picha na Janeth Mushi.
Muktasari:
- Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (Tawja) Mkoa wa Arusha, kimesema uoga wa wananchi katika kuripoti udhalilishaji wa mitandaoni kwa wanawake na watoto kumechangia kuendelea kukua kwake.
Arusha. Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (Tawja) Mkoa wa Arusha, kimetoa elimu kuhusu kupinga ukatili wa kijinsia hasa udhalilishaji wa kimtandao na kuwahamasisha watu kuripoti kwenye vyombo vya sheria matukio hayo yanapojitokeza.
Elimu hiyo imetolewa leo, Ijumaa Desemba Mosi, 2023 katika Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira, kilichopo wilayani Arumeru, Mkoa wa Arusha.
Mafunzo hayo ni sehemu ya kampeni maalumu ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambapo pia chama hicho kilitoa mfano wa namna ya kuendesha kesi mahakamani.
Mratibu wa Tawja Mkoa wa Arusha, Maria Sambo amesema wameamua kutoa mafunzo hayo kwa kuwapitisha wanafunzi hao kwenye sheria mbalimbali za makosa ya kimtandao kwa kuwa kumekuwa na makosa mengi ya kimtandao ikiwemo ya udhalilishaji ila wengi wamekuwa waoga kuyaripoti.
"Tunaona makosa mengi ya kimtandao, video nyingi tuona zinatumwa huko, picha za udhalilishaji...tumekuja kwenu wanafunzi mzifahamu sheria ili siku moja kama wanasheria, mjue ni njia gani mtatumia kudeal na hizo kesi," amesema.
"Tunaona wengi wamekuwa waoga kuripoti matukio ya udhalilishaji mitandaoni hivyo nawahimiza waathirika wa matukio hayo kuyaripoti katika vyombo vya sheria ili waweze kuondokana na athari zinazoweza kujitokeza ikiwemo kujiua," ameongeza
Naye Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Joachim Tiganga, amesema mafunzo hayo yamelenga kuamsha ari ya wanajamii kupambana na mambo ya kikatili yanayofanyika mtandaoni dhidi ya vijana.
Amesema kukabiliana na ukatili wa kijinsia hasa wa mtandaoni siyo jambo rahisi kulishughulikia kutokana na kukua kwa teknolojia, hivyo elimu ya matumizi sahihi ya mitandao inapaswa kutolewa kwa makundi yote.
"Kwa namna ilivyo hakuna namna jamii yetu itajitenga na mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea lakini tunatakiwa kushiriki kwenye mabadiliko hayo huku tukichukua tahadhari na kuwakinga vijana na watoto wetu ambao wanaweza kudanganywa na wakadanganyika, lakini pia wakapoteza ndoto walizo nazo,” amesema Jaji huyo.
Mmoja wa wanafunzi wa sheria chuoni hapo, Joseph Raphel amesema mafunzo hayo yameonyesha ni jinsi gani ukatili wa kijinsia unavyofanyika mitandaoni, na kwamba yatasaidia kujenga wanafunzi katika kutumia matumizi sahihi ya mitandao.