Tawla yataka maboresho ya Sheria ya Usalama barabarani

Muktasari:
- Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla) kimesema kuna haja ya kufanyika kwa maboresho ya Sheria ya Usalama Barabarani, ili kuepusha majanga ya ajali yanayo yanayogharimu maisha ya watu, kusababisha ulemavu na hata kudidimiza uchumi.
Dar es Salaam. Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla) kimesema kuna haja ya kufanyika kwa maboresho ya Sheria ya Usalama Barabarani, ili kuepusha majanga ya ajali yanayo yanayogharimu maisha ya watu, kusababisha ulemavu na hata kudidimiza uchumi.
Hayo yamebainishwa jana Oktoba 2, jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho, Tike Mwambipile wakati wa semina ya siku moja kwa wadau na wana mtandao wa asasi za kiraia wanaoshawishi maboresho ya sheria ya usalama barabarani.
Mwambipile amesema kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), watu 1.5 milioni hufariki duniani kila mwaka kutokana na ajali hizo za barabarani.
Amesema pia ajali za barabarani hugharimu nchi husika karibu asilimia tatu ya pato la taifa na asilimia 93 ya ajali hizo hutokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati ikiwemo Tanzania.
"Pamoja na takwimu hizo bado katika miaka mitano ya kufanya kazi kwenye eneo hilo la usalama barabarani tunajivunia kusomwa kwa mara ya kwanza kwa mswada wa mapendekezo ya sheria ya usalama barabarani ambao umezingatia mapendekezo matano kati ya sita ambayo tumekuwa tukiyasemea kwa muda mrefu," amesema Mwambipile.
Hata hivyo, alisema pamoja na mafanikio hayo wanaishauri Serikali kuliangalia sula la usalama barabarani kuwa ni agenda mtambuka na shirikishi inayomgusa kila mmoja na sio suala la polisi na taasisi zake pekee.
"Tunaiomba pia Serikali na wadau wengine wa maendeleo nchini kuiwezesha sekta hii ya usalama barabarani na sio kutegemea wafadhili wa nje tu," amesema.
Naye mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Evance Gingo alisema ili kuhakikisha muswada ulipo bungeni unapita, amewataka waandishi wa habari kuendelea kuandika habari za usalama barabarani zenye ubunifu na ushawishi.