TPDC kutafiti mafuta, gesi Bonde la Eyasi

Sindi Maduhu, Meneja wa Mradi wa Utafiti Bonde la Eyasi Wembere akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) muda mfupi baada ya kuwasilisha taarifa ya kuanza kwa utafiti wa mafuta na gesi asilia mkoani Simiyu. Picha na Samira Yusuph 

Muktasari:

Bonde la Eyasi Wembere liko katika mkondo wa Bonde la Ufa ambalo pia linapatikana katika nchi jirani za Kenya na Uganda ambazo tayari zimeanza miradi ya utafiti wa mafuta umefanyika huku Uganda wakiwa tayari wameanza kuchimba mafuta.

Bariadi. Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linatarajia kuanza utafiti wa kijiofizikia (2D seismic) ifikapo June 2023 kutambua maeneo ya uchimbaji wa visima virefu vya utafiti wa mafuta na gesi asilia.

Utafiti huo unalenga mikoa mitano ya Simiyu, Singida, Tabora, Manyara na Arusha, hasa katika maeneo yanayopitiwa na bonde la Eyasi Wembere. 

Hayo yameelezwa leo Aprili 27, 2023 na Meneja Mradi wa Utafiti Bonde la Eyasi Wembere, Sindi Maduhu alipokuwa akitoa taarifa ya mradi huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahya Nawanda.

Amesema utafiti huo utakaoanza mwezi June, 2023 na kukamilika Novemba, 2023 utahusisha laini lenye urefu wa kilomita 260.

Eneo linalotarajiwa kutumika katika utafiti wa mafuta na gesi asilia kwa Mkoa wa Simiyu ni Kata za Nyalanja, Bukundi, Mwamalolo, Mwamanimba na Mwanjolo wilayani Meatu.

"TPDC inaomba utayari na ushirikiano kutoka kwa wananchi na vyombo vya usalama kwa sababu utafiti huu utahusisha mitambo mikubwa ya kuchukua taarifa za miamba kwa njia ya mitetemo,"Amesema Maduhu.

Amesema tafiti mbili zimefanyika, moja mwaka 2015 na nyingine ya mwaka 2019 uliohusisha uchorongaji wa mashimo kuangalia aina ya miamba iliyopo katika eneo la Meatu Simiyu, Igunga Tabora na Singida ilionyesha viashiria vya uwepo wa mafuta.

"Mwaka 2021/2022 sampuli 1136 zilichukuliwa na kupelekwa maabara nchini Marekani kuchakatwa na kubainisha zaidi viashiria vya mafuta, hadi sasa inatarajiwa kuwa mapema June 2023 taarifa rasmi itatolewa ya hali ya viashiria vya mafuta vilivyopo," amesema Maduhu.

Meneja Mawasiliano wa TPDC, Marie Msellemu amesema wenyeji wa maeneo hayo watanufaika kwa njia mbalimbali ikiwemo ajira na shughuli zingine za kiuchumi iwapo mafuta au gesi yatathibitika kuwepo maeneo yao.

"Hakuna uharibifu wa mazingira katika mradi huu na umiliki wa ardhi utabaki chini ya wenyeji na mauzo ya bidhaa za mradi yataboresha upatikanaji wa huduma za kijamii," Amesema Msellemu.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahya Nawanda amesema uwepo wa mafuta au gesi katika maeneo hayo ukithibitika, ni dhahiri hali za kiuchumi, miundombinu na huduma zitaimarika na kuboreka.

"Simiyu tupo tayari na tuna uhakika siyo tu wa kunufaika kupitia sekta ya kilimo, ufugaji, biashara na ujasiriamali. Tutawahudumia wageni na wawekezaji watakaokuja kuwekeza katika maeneo yote ya kiuchumi mkoani kwetu,” amesema Dk Nawanda.