Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TRA Kilimanjaro yavuka lengo ukusanyaji mapato

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kisare Makori akiwa na  Meneja wa TRA, Mkoa wa Kilimanjaro, James Jilala wakati akikata utepe katika  uzinduzi wa wiki ya shukrani kwa mlipa kodi,  iliyofanyika katika viwanja vya Ofisa za TRA. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro imekusanya Sh263.1 bilioni kwa mwaka wa fedha 2022/23, zaidi ya lengo lillilokusidiwa la kukusanya Sh257.84 bilioni kwa kipindi kilichopita.

Moshi. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Kilimanjaro imekusanya Sh263.1 bilioni kwa mwaka wa fedha 2022/23 ambayo ni zaidi ya asilimia 102 ya lengo lilolokusidiwa la Sh257 .84 bilioni kwa kipindi kilichopita.

 Akizungumza leo, Novemba 27, 2023 katika uzinduzi wa wiki ya shukrani kwa mlipa kodi, Meneja wa TRA Kilimanjaro, James Jilala amesema mafanikio hayo yanatokana uwajibikaji wa watumishi pamoja na walipa kodi kujitambua na kulipa kodi kwa wakati, bila kushurutishwa.

Jilala amesema katika mwaka wa fedha unaoendelea wa 2022/2023, wameshakusanya Sh71.25 bilioni kati ya Julai hadi Oktoba 2023, ambapo amesema ni asilimia 72 ya lengo la kukusanya Sh76.77 bilioni katika kipindi hicho ikiwa lengo ni kukusanya Sh240.8 bilioni.

"Mkoa wa Kilimanjaro kwa kipindi kilichopita cha awamu ya pili mwaka 2022/2023 tulikusanya Sh257.84 bilioni na tulifanikiwa kukusanya Sh263.1 bilioni ambayo ni sawa na asimilia 102," amesema.

Jilala amesema pamoja na mafanikio hayo, wanakabiliana na changamoto ya kudhibiti biashara za magendo katika maeneo ya Moshi vijijini hasa Chekereni na Kahe ambako wafanyabiashara wasio waadilifu wamekuwa wakivusha bidhaa mbalimbali, hali inayochangia upotevu wa mapato.

Hata hivyo, amesema mikakati ipo kukabiliana na hali hyo kwa kushirikiana na taasisi za Serikali na wafanyabiashara waaminifu.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kisare Makori amevitaka vyombo vinavyojihusisha na masuala ya doria kuongeza nguvu maeneo ya mipakani, kudhibiti wafanyabiashara wanaofanya biashara za magendo na kuikosesha Serikali mapato.

"Kuna watu wanaofanya biashara za miamala, wanaleta bidhaa au huduma, lakini hawalipi kodi wanatumia njia zisizo rasmi. Niwaombe wafanyabiashara wetu, tuwe na uzalendo na nchi yetu na tufuate sheria, ili tutoe mchango wetu katika ukuaji wa nchi wetu.

"Tunafahamu mpaka wetu wa mkoa, hasa upande wa Rombo, tunapakana na nchi jirani, vipo vipenyo zaidi ya 376 ambavyo baadhi ya watu wasio na uzalendo na nchi yao wanatumia kuingiza bidhaa kukwepa kodi, naomba tufanye biashara zetu kwa kufuata sheria na kulipa kodi," amesema.

Pamoja na mambo mengine, amewataka wafanyabiashara wa wilaya hiyo kuhakikisha wanapotoa huduma wanatoa risiti za mashine za EFD na wale wanaopata huduma kudai risiti ili kuiongezea Serikali azma yake ya kukusanya mapato kwa maendeleo ya Taifa.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa wilaya hiyo, msemaji wa jumuiya ya wafanyabiashara mkoani hapa, Issihaka Juma amesema wataendelea kushirikiana na Serikali kutoa taarifa mbalimbali, ili kuhakikisha kodi zinalipwa kwa wakati.

"Wafanyabiashara tumetambua umuhimu wa kulipa kodi, ndiyo maana tunaona mapato yanapanda siku hadi siku kutokana na elimu kwa mlipa inayotolewa na TRA, kama jumuiya tutaendelea kushirikiana hata kutoa taarifa mbalimbali mtakazohitaji ili kuhakikisha kodi inakusanywa kadri inavyotakiwa," amesema.