TRA Tabora yakusanya mapato kwa asilimia 106 robo mwaka
Mfanyabiashara Mohamed Salum (kushoto) akipokea tuzo ya mshindi wa jumla wa tatu kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Saida Mtondoo, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian, kulia nimeneja wa TRA mkoa wa Tabora, Thomas Masese na wa pili kushoto ni mwenyekiti wa wajasiriamali mkoa wa Tabora, Ashura Mwazembe. Picha na Robert Kakwesi
Muktasari:
TRA Tabora yavuka lengo la.makusanyo robo ya kwanza mwaka wa fedha 2022/23 kwa kukusanya kwa asilimia 106.
Tabora. Mamlaka ya Mapato (TRA) mkoani hapa imetangaza kuvuka asilimia 100 ya makusanyo katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha ambao imepewa lengo la kukusanya Sh25.67 bilioni.
Akizungumza katika siku ya mlipakodi leo Jumamosi Novemba 26, Meneja wa TRA mkoani Tabora, Thomas Masese, amesema robo ya kwanza Julai hadi Septemba 2022, wamekusanya Sh6.16 bilioni sawa na asilimia 106 ya lengo lililowekwa la kukusanya Sh5.84 bilioni.
Amesema ufanisi huo ukilinganisha na robo ya kwanza ya mwaka 2021/22 ni kuwa kumekuwa na ongezeko la kodi kiasi cha Sh1.74 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 39.
Amesema mafanikio hayo ni kutokana na ushirikiano uliopo baina ya Mamlaka na wafanyabiashara, akisema ushirikiano unazidi kuimarika.
"Wamekuwa wakitupa ushirikiano mkubwa pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali," amesema.
Amezitaja changamoto zilizopo kuwa ni kubwa katika matumizi ya mashine za kielektroniki (EFD) kwa baadhi ya wafanyabiashara kutokuwa waaminifu, wengine kutotoa risiti au kutoa risiti pungufu ya mauzo halisi na baadhi wanaostahili kumiliki mashine hizo kushindwa kufanya hivyo.
Akizungumza katika mkutano huo, Makamu mwenyekiti sekta ya Viwanda wa Chama cha wafanyabiashara, Viwanda na kilimo (TCCIA), Donatus Rupoli amesema hali ya kukimbiana imefutika miongoni mwa wafanyabiashara na watumishi wa TRA kutokana na kuaminiana na ushirikiano uliopo hali inayochangia mapato kuongezeka.
Ameipongeza TRA kwa mabadiliko na kwamba Kunapokuwepo haja ya mashauriano pande mbili hukutana na kuzungumza na kuupongeza uongozi wa TRA na watumishi kwa ushirikiano.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya usafirishaji ya NBS, Mohamed Hamduni, amesema kuwa TRA wamefanya mabadiliko makubwa katika mahusiano na wafanyabiashara na kufanya mapato kuongezeka.
Ameeleza kuwa zamani ilikuwa ni chui na paka, lakini sasa ushirikiano wao na TRA ni kama chanda na pete na kupongeza kwa ushirikiano huo.