TRA yamtangaza mlipakodi bora mwanamke mwaka 2023

Muktasari:

  • Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imemtambua na kumzawadia mwanamke ambaye ameibuka kuwa mlipaji kodi namba moja nchini Tanzania mwaka 2023.

Dar es Salaam. Wakati wanawake nchini wakiungana na wenzao duniani kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imemtangaza Mtendaji wa Kampuni ya Utalii ya Zara Internation Travel Agency, Zainab Ansell kuwa mlipaji kodi bora mwanamke Tanzania.

Mwanamke huyo ametangazwa leo Machi 8, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya wanawake wa TRA kusherehekea siku hiyo .

Katika hafla hiyo, wanawake wa TRA wamehamasishwa kufanya kazi kwa kuzingatia weledi ili wananchi nao wahamasike kulipa kodi kwa hiari.

Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Mcha Hassan Mcha amesema wamefurahishwa na mamlaka hiyo kumtambua na kumzawadia mwanamke huyo, ambaye ameibuka kuwa mlipaji kodi namba moja nchini.

“Hongera sana Zainabu kwa kutajwa kuwa kinara wa walipakodi wanawake Tanzania kwa mwaka 2023, hii ni hatua kubwa na yenye umuhimu mkubwa katika kuleta mabadiliko na kuleta mwanga kwa wanawake katika ulimwengu wa kodi,” amesema Mcha.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, akimwakilisha Zainab, Leyla Lakhan ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Utalii ya Zara Internation Travel Agency, amesema wataendelea kulipa kodi ili mwakani wapate zawadi nyingine ya kuwa mwanamke bora.

“Siri ya kuwa mlipa kodi namba moja Tanzania ni kwamba tunafanya kazi kwa bidii na tunalipa kodi kwa wakati kama inavyotakiwa,” amesema Lakhan.

Awali, Mcha amewahamasisha wanawake kuwa na maadili mema ya kazi yatakayowajengea uhusiano mzuri na wateja wao ili kuongeza ari ya ulipaji wa kodi kwa hiari.

Amesema wanawake hao watakapokuwa na maadili mazuri ya kazi, wataendelea kuweka taswira nzuri huku wakijenga uhusiano mzuri na kuongeza ari ya ulipaji kodi kwa hiari na kwa wakati.

“Sote tunakumbuka kuwa wanawake ni jeshi kubwa, hivyo mkisimama kidete katika hii mtaleta mabadiliko makubwa katika jamii yetu na kuiwezesha TRA kutimiza malengo yake ya ukusanyaji kodi Kwa maendeleo ya Taifa,” amesema Mcha.

Amesema TRA imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanawake watumishi wanapata stahiki na haki zao kama ilivyoainishwa kwenye sheria na kanuni za utumishi.

Kaimu Mkurugenzi Rasilimali watu na Utawala, Renalda Lyimo amesema wanatambua juhudi zinazofanywa na wanawake wa mamlaka hiyo katika kuhakikisha malengo ya taasisi yanafikiwa kwa kukusanya kodi ya Serikali kwa ufanisi.

“Kauli mbiu ya mwaka huu imebeba maudhui yanayodhihirisha mchango mkubwa wa wanawake katika uchumi wa nchi na maendeleo ya jamii kwa ujumla,” amesema Lyimo.