Tucta, Serikali kujadiliana maslahi ya wafanyakazi

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Henry Mkunda.
Muktasari:
- Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) limesema maadhimisho ya Mei Mosi ya mwaka huu yamekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa madai ya wafanyakazi yamesikilizwa na kwamba litaendelea kujadiliana na serikali ili kuboresha maeneo mengine.
Dar es Salaam. Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) limesema maadhimisho ya Mei Mosi ya mwaka huu yamekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa madai ya wafanyakazi yamesikilizwa na kwamba litaendelea kujadiliana na Serikali ili kuboresha maeneo mengine.
Hayo yamebainishwa leo Mei 5, 2023 jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Tucta, Said Wamba wakati akitoa tathmini ya sherehe hizo zilizofanyika kitaifa mkoani Morogoro, mgeni rasmi akiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Katika sherehe hizo, Rais Samia aliahidi kurejesha nyongeza ya kila mwaka ya mishahara kwa wafanyakazi, hata hivyo hakubainisha ongezeko hilo litakuwa la kiasi gani ikiwa ni mbinu ya kuepusha wafanyabiashara kupandisha bei ya bidhaa mara tangazo la kupanda kwa mishahara linapotolewa.
Wamba amesema Rais Samia ametoa nafasi kwa Serikali kukutana na Tucta kujadiliana juu ya masuala mbalimbali ya wafanyakazi, amesema watatumia nafasi hiyo kusukuma utekelezaji wa masuala mengine ya muhimu kwa wafanyakazi.
"Vyama vya wafanyakazi ni vyombo vya majadiliano na siyo vya mapambano kama wengine wanavyodhani. Mazungumzo yakishindikana basi hatua inayofuata ndiyo mapambano. Lakini hatuwezi kuanza na mapambano wakati hatujafanya majadiliano.
"Kwa hiyo tunajipanga kwa majadiliano na serikali na tutatumia nafasi hiyo kuwasilisha hoja za wafanyakazi kama vile masuala ya mishahara, kodi za wafanyakazi zipunguzwe, masuala ya bima na mikataba ya kazi," amesema Wamba.
Ameipongeza Serikali kwa kuwa sikivu katika kushughulikia maslahi ya wafanyakazi huku akieleza kwamba ni katika awamu ya sita, watumishi wameongezwa mishahara yao baada ya takribani miaka saba kupita.
Kuhusu mishahara ya wafanyakazi wa sekta binafsi, Wamba amesema mwaka 2022 serikali iliongeza kima cha chini, hata hivyo alisema Bodi za Mishahara zilipendekeza kima cha chini cha muda mfupi kwa sababu hawakupata muda wa kufanya utafiti wa hali ya maisha.
"Kwenye majadiliano yetu na serikali, tunakwenda kusukuma hizi Bodi zipewe muda zaidi wa kutathmini kima cha chini cha mishahara kwenye sekta binafsi hapa nchini," amesema Wamba.
Kiongozi huyo wa Tucta amesisitiza kwamba wafanyakazi wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii ili waongeze tija katika maeneo yao na kwamba hilo litawapa nguvu Tucta ya kudai nyongeza ya mishahara.
"Tunasisitiza hili jambo ili wafanyakazi wajue hiki tunachokidai kinatokana na jasho lao," amesema Wamba wakati akizungumza na vyombo vya habari hapa Tanzania.