Tume: Viongozi wa halmashauri wasikamate watuhumiwa

Mwenyekiti Tume ya Haki Jinai, Jaji Mstaafu, Othman Chande.
Muktasari:
- Tume ya haki jinai nchini imetoa mapendezo kuwataka viongozi ya halmashauri kuacha kukamata watuhumiwa na suala hilo likibaki mikononi mwa polisi.
Dar es Salaam. Tume ya kuboresha mfumo na taasisi za haki jinai nchini imependekeza kuwa mamlaka ya kipolisi ya kukamata na kuweka mtuhumiwa kizuizini waliyonayo wakurugenzi wa halmashauri, maofisa watendaji wa kata yaondolewe na jukumu hilo liachwe kwa Jeshi la Polisi.
Mapendekezo hayo yamewasilishwa leo Jumamosi Julai 15, 2023 Ikulu, Dar es Salaam na Mwenyekiti Tume ya Haki Jinai, Jaji Mstaafu, Othman Chande.
Amesema tume imebaini kuwa mamlaka ya kukamata imetolewa kwa taasisi nyingi na kwa watu wengi kuvishwa kofi za kipolisi.
“Tume imebaini mamlaka ya sheria za Serikali za Mtaa, Halmashauri pia zinapitisha sheria ndogo makosa ya jina na kuna vifungu za sheria hiyo vinawapa mamlaka ya kipolisi wakurugenzi wa halmashauri na watendaji wa kata ya kukamata na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa.
“Sheria hizo hazitoi mipaka na haziwapi watu nafuu ya kuomba rufani ya maamuzi hayo.
“Mapendekezo yetu mamlaka ya kipolisi ya kukamata na kuweka mtuhiwa kizuizini waliyonayo wakurugezi wa halmashauri na maafisa watendaji wa kata yaondolewe kwenye sheria hizo na jukumu hilo kuachwa mikononi mwa jeshi la polisi” amesema Chande.
Tume ya kuboresha mfumo na taasisi za haki jinai nchini iliundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Januari 2023 na kuanza kazi Februari Mosi.