Uchaguzi CCM Morogoro waingia dosari

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Chief Sylvester Yaredi

Muktasari:

 Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Morogoro Mjini, kimetengua kisha kuamuru kurudiwa kwa shughuli ya uchukuaji wa fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho na jumuiya zake.


Morogoro. Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Morogoro Mjini, kimetengua kisha kuamuru kurudiwa kwa shughuli ya uchukuaji wa fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho na jumuiya zake.

Ni baada ya kata nane kati ya 29 kubainika kuwa na dosari kwenye shughuli hiyo ya awali ya uchukuaji fomu kwa baadhi ya wagombea kudaiwa kupanga safu ya uongozi mkoani humo.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa, Julai 22, 2022, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Chief Sylvester Yaredi amesema kata nane kati ya 29 zitarudia uchukuaji fomu baada ya kamati ya siasa ya Halmashauri Kuu CCM wilaya kujiridhisha kwa dosari nyingi.

Yaredi amesema baada ya vikao vya kuchambua majina na sifa za wagombea, wamebaini dosari na kukiuka taratibu za chama wakati wa uchukua wa fomu.

Ametaja kata hizo ambazo Wanaccm watachukua fomu ni Mkundi, Boma, Mji Mpya, Sabasaba, Chamwino, Kihonda, Mazimbu na Kingo.

Mkazi wa Manispaa ya Morogoro, Farida Abubakari amepongeza hatua hiyo kwa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM kuchukua uamuzi wa uchukuaji fomu baada ya kubaini dosari ambazo zinatia doa chama tawala.

“CCM wilaya kimeonyesha ukomavu kwa kuchukua hatua baada ya kuona dosari kwa kata nane,” amesema na kuongeza:

“Mimi naona CCM sio chama cha watu kujificha kwa kupanga safu kwa kujuana na hatua hii vyama vingine navyo viige mfano endapo itabaini uhuni wa baadhi ya wagombe ili kujijengea uaminifu kwa jamii.”

Naye Salumu Majali amesema hiyo ndio nafasi kwa wanaccm ambao hawakuchukua fomu awali kuomba uongozi.

“CCM wilaya isiishe katika kurudiwa kwa uchukuaji wa fomu tu bali intelejinsia yao iwabaini pia viongozi waliosababisha kutokea kwa dosari na wawajibishwe kulinda heshima ya chama ili kuepuka kuwa na viongozi sio na maadili kwa taifa,” amesema Salumu.

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo alikwisha kutoa maelekezo ya kuchukuliwa hatua kwa wale wote wanaopanga safu au kucheza michezo michafu ili kuhakikisha wanashinda “kukata majina yao.”