Uchunguzi kifo tata cha mwanafunzi Udom bado

Mwanafunzi, Nusura Hassan Abdalla enzi za uhai wake.

Muktasari:

  • Baada ya Jeshi la polisi kuita wananchi wenye taarifa zitakazosaidia uchunguzi wa haraka kuhusu taarifa za kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) Nusura Abdallah, limesema uchunguzi huo haujakamilika.

Dodoma. Jeshi la Polisi nchini limesema halijakamilisha uchunguzi wa taarifa za kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Nusura Abdallah na kuwataka wananchi wawe na subira.

 Hayo yameelezwa leo Mei 15, 2023 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime wakati alipoulizwa na Mwananchi kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma.

Akimzungumzia kuhusu uchunguzi wa kifo cha mwanafunzi huyo aliyekuwa anasoma shahada ya kwanza ya Sanaa katika Elimu, Misime amesema baada ya Jeshi kukamilisha uchunguzi wake litatoa taarifa.

“Mtakumbuka katika taarifa yangu nilisema tukikamilisha tutawapa taarifa lakini hatujakamilisha na nisingetaka kuzungumza lolote kwasababu naweza nikawawekea maneno wanaochunguza wakaja na taarifa siyo za kiuchunguzi, naomba tuvute nsubira,”alieleza Misime.

Aidha amesema jeshi hilo linawashikilia watu watatu kufuatia mauaji ya Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Nyangoto, Dk Isack Sima aliyeuawa na watu wasiojulikama Mei 3, 2023 Tarime Vijijini.

Katika hatua nyingine jeshi hilo linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya Milembe Seleman (43) Mfanyakazi wa kitengo cha Ugavi katika kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu (GGM) ambaye alikutwa na majeraha ya kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo kichwani, usoni na mikononi ambapo kiganja kimoja cha mkono kiliondolewa.

“Hata hivyo mtuhumiwa wa nne baada ya kupata taarifa za kukamatwa wenzake na askari kufika nyumbani kwake, Mei 6, 2023 alijihukumu kwa kujinyonga kwa kutumia mkanda wa suruali katika pori la hifadhi ya Buhindi Sengerema, mtuhumiwa huyo amejulikana kwa jina la Pastory Lugodisha,”amesema Misime.