Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uchunguzi waanza ununuzi majokofu ya nyumbani kuhifadhia damu

Mkurugenzi wa huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe  – Tamisemi, Dk Rashid Mfaume akiangalia moja ya jokofu la nyumbani lililonunuliwa kuhiffadhia damu katika Kituo cha Afya Mwalugulu Msalala Mkoa Shinyanga. Kulia ni mwonekano wa ndani wa jokofu na kuhifadhia damu. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Mkurugenzi awataka watumishi wa afya kuzingatia taratibu za kiutumishi ambazo zitaepusha mambo kama hayo kutokea.

Mwanza. Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama, mkoani Shinyanga imeanza uchunguzi kubaini wahusika walionunua majokofu ya matumizi ya nyumbani kwa ajili ya kuhifadhia damu.

Aprili 10, 2024 Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Rashid Mfaume alibaini ukiukwaji wa manunuzi ya vifaatiba ikiwemo ununuzi wa majokofu mawili ya kuhifadhia damu katika kituo cha afya Mwalugulu katika halmashauri hiyo.

Akiwa kwenye ziara kukagua na kuangalia usimamizi shirikishi wa shughuli za huduma za afya ndani ya kituo hicho, Dk Mfaume alibaini majokofu yaliyonunuliwa kila moja kwa Sh3.8 milioni ni kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Pia alibaini mashine ya dawa za usingizi (Anaesthetic Machine) iliyonunuliwa kwa Sh140 milioni imepokewa katika kituo hicho bila kukaguliwa.

“Tunaponunua vifaa vya hospitali ni tofauti na  vingine, tunakuwa na viwango vyetu ambavyo tunaainisha wakati wa kuagiza, hata yale majokofu ambayo tunahifadhia damu si kama haya ambayo tunahifadhia matunda, tunahifadhia ubwabwa nyumbni, yale yanakuwa mazuri kufanya ile damu iendelee kuwa na ubora ule wa viwango vya joto na vingine,” alisema Dk Mfaume alipozungumza na gazeti hili.

Dk Mfaume alisema majokofu hayo yalitarajiwa kutumiwa mwezi ujao baada ya huduma za damu salama kuanza katika kituo hicho cha afya.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala, Hamisi Katimba bila kutaja hatua gani za awali zilizochukuliwa, alisema tayari uchunguzi umeanza na watakaobainika watachukuliwa hatua za kinidhamu.

“Jambo hilo linashugulikiwa kujua tatizo limetokea wapi na changamoto ilitokea wapi mpaka badala ya pharmaceutical refrigerator (jokofu la kuhifadhia vifaatiba) likanunuliwa lile, kwa hiyo hatua za kiuchunguzi na kinidhamu za halmashauri zimeanza kuchukuliwa,” alisema.

“Wito wangu kwa watumishi wa afya suala la msingi ni kuzingatia taratibu za kiutumishi ambazo zitaepusha mambo kama hayo kutokea, watu kama wangekuwa makini hilo  lisingeweza kutokea hapa.

“Naamini katika taratibu za uchunguzi zilizochukuliwa zitaanza kutoa ushauri ili kuzuia changamoto zisije kutokea tena,” alisema.


Tofauti za majokofu

Kwa mujibu wa Ofisa mhamasishaji wa damu salama Kanda ya Kati, Bernadino Medaa kuna utofauti mkubwa kati ya majokofu ya matumizi ya nyumbani na yale ya kitabibu kwa ajili ya kuhifadhia damu kutokana na viwango vya kuhifadhi joto na baridi kutofautiana.

“Utofauti ni mkubwa sana. Kuna kiwango maalumu cha joto na ubaridi wa kuhifadhi damu. Ukizidisha au kupunguza ubaridi tayari zile seli hai zinakufa na zinakuwa hazifai kwa matumizi,” alisema na kuongeza:

“Ni bora kutumia friji ya kitabibu kwa sababu ya ule ubora wa kuhifadhi damu yenyewe, yale ya nyumbani ni kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, unaweza ukaweka maji, nyama, mboga; lakini damu yenyewe ina utaratibu wake tangu inapochukuliwa kwa mtu.”

Alisema, “inabidi kwanza ipoe kidogo kama saa moja halafu ndiyo inaruhusiwa kuwekwa kwenye friji na ile friji yenyewe inatakiwa ikae kwenye jotoridi digrii mbili hadi 10.

“Lakini mafriji ya nyumbani ukienda kulipima unakuta jotoridi 11, 12 mpaka 13, ukiweka damu humo kuna uwezekano wa zile seli hai ambazo zipo kwenye damu zikafa.”

Alisema hata mpangilio wa ndani wa majokofu  umetofautiana.

“Mafriji ya damu huwa yana vitrei fulani ambavyo hata ukipanga damu zinakaa kwa mpangilio maalumu lakini friji za nyumbani zimetengenezwa kwa ajili ya kuwekea vitu vya kula kwa hiyo hata mpangilio wa ndani hauko sawa,” alisema.

Alisema inashauriwa damu zikae kwenye jokofu maalumu zilizoainishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) au wataalamu wa afya kwenye nchi husika ili damu isiharibike ili ikienda kwa mgonjwa iende kumsaidia.

Alisema damu ikiganda hairuhusiwi kwenda kwa mgonjwa.