Ujumbe wa Lowassa kwa Chadema, CCM huu hapa

Freddy Lowassa (kulia) akipokea wazazi wake walipowasili uwanja wa ndege wa Arusha leo. Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

Leo Jumamosi, Edward Lowassa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, amezungumza na wana CCM wa Monduli mkoani Arusha na kueleza mambo mbalimbali juu ya wana CCM na chama chake cha zamani cha Chadema

 


Monduli. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amewaomba Watanzania waliompigia kura katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka 2015 kumuunga mkono, Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Lowassa aliyekuwa mgombea urais katika uchaguzi huo kupitia Chadema na kuungwa mkono na vyama washirika vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NLD, NCCR-Mageuzi na CUF alipata kura milioni sita huku Dk John Magufuli wa CCM akipata milioni nane.

Hata hivyo, Lowassa ambaye alijiunga na Chadema Julai 28, 2015 akitokea CCM, Machi Mosi 2019 alitangaza kurudi CCM.

Leo Jumamosi, Machi 9, 2019 Lowassa amekwenda Monduli mkoani Arusha ambako anakabidhiwa kadi ya uanachama na amezungumza na mamia ya wanachama waliojitokeza kumpokea.

“Nimerudi nyumbani msiniulize nimerudi kufanya nini, nimerudi nyumbani,” amesema Lowassa ambaye amesindikizwa na mke wake, Regina na mwanaye Fred

Akiendelea kuzungumza amesema, “Kwenye uchaguzi nilipata kura zaidi ya milioni sita si haba, naomba wote walionipigia kura tumuunge mkono Rais John Magufuli.”

“Nampongeza Rais John Magufuli kwa ushawishi wake ambao umenifanya nimerudi nyumbani,” amesema.

Huku akishangiliwa, Lowassa amesema, “Kwa Chadema nawashukuru viongozi na wanachama sana, sitaki watu wengine waniwekee maneno mdomoni.”

Endelea  kufuatilia Mwananchi kujua kinachojiri huko