Ukame waua mifugo 62,500 Simanjiro

Muktasari:

Hali ya ukame inayoendelea wilayani Simanjiro mkoani Manyara imesababisha mifugo mbalimbali ikiwemo ng'ombe, kondoo, mbuzi na punda kufa.

Simanjiro. Mifugo 62,593 imekufa wilayani Simanjiro mkoani Manyara kutokana kukosa maji na malisho baada ya ukame kuvikumba vijiji mbalimbali katika wilaya hiyo.

 Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Sendeu Laizer ameyasema hayo Januari 13 kwenye kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo.

Sendeu ameitaja mifugo hiyo iliyokufa kuwa ni ng'ombe 35,746, kondoo 15,136, mbuzi 10,033 na punda 1,670.

Amesema katika kipindi hiki hali ya mifugo katika maeneo mengi ya Simanjiro siyo ya kuridhisha kutokana na uhaba wa maji na malisho.

Amesema ufuatiliaji na ukusanyaji wa taarifa za vifo vya mifugo kutokana na athari za ukame unaendelea katika vijiji vyote.

"Hali hii imesababisha baadhi ya mifugo kufa na wafugaji wengi kuhama na kurundika katika maeneo machache yenye maji na malisho," amesema Sendeu.

Mbunge wa jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amesema kutokana na ukame huo jamii nyingi zimeingia kwenye umaskini kutokana na mifugo yao kufa.

Ole Sendeka amesema kwa sababu ya ukame uliopo nchini baadhi ya wafugaji wamehamisha mifugo yao nje ya nchi ili zipate malisho.

Diwani wa kata ya Naisinyai, Taiko Kurian ametoa ombi kwa Serikali kuruhusu mifugo kuingia ndani ya ukuta wa madini ya Tanzanite ili kupata malisho.

"Mifugo ni benki ya jamii za kifugaji sasa inapokufa kwa ukame inakuwa tatizo tunaiomba Serikali iruhusu mifugo kuingia ndani ya ukuta wa madini ya Tanzanite kwani haitadhiriana," amesema Taiko.


Simanjiro yapitisha Sh25.2 bilioni

Wakati huo, madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro wamepitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya Sh25.2 bilioni kwa ajili ya mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Ofisa mipango wa halmashauri hiyo, Heri Kuria amesema bajeti hiyo imelenga kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya elimu, afya, maji na miundombinu.

Amesema katika bajeti ya 2022/2023 halmashauri hiyo itatekekeleza miradi mbalimbali na katika bajeti hiyo itaongeza ujenzi wa madarasa ya shule za msingi 20, shule mpya ya sekondar na kituo cha afya.