Ukusanyaji takwimu za kilimo sasa kidijitali

Muktasari:

  • Kuanzia sasa, Tanzania itaepukana na na mfumo wa zamani wa kukusanya takwimu za uzalishaji nchini kwa kukadiria, baada ya maofisa kilimo nchini kupata mafunzo ya matumizi ya ukusanyaji wa takwimu hizo kidigitali.

Mbeya. Wakati Tanzania na Morocco zikishirikiana kuzindua mfumo mpya wa ukusanyaji takwimu kidijitali, maofisa kilimo 120 na wasaidizi 24, wamejengewa uwezo na wa namna ya kutumia simu janja kupata takwimu za uzalishaji nchini.

Inaelezwa kuwa, matumizi ya mfumo huo yatasaidia Taifa kujipanga na kuwa na uhakika wa chakula, kwani takwimu zitahusu uzalishaji wa mazao mbalimbali.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi Digital leo Jumamosi Desemba 2, 2023, Mtafiti wa udongo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (Tari) Uyole, jijini hapa, Fedrick Mlowe amesema lengo ni kuwezesha maofisa kilimo kuondokana na mfumo wa zamani wa kukadiria uzalishaji.

“Tanzania na Morocco tumezindua mfumo  wa kukusanya takwimu kwa njia ya kidigitali kwa kutumia simu janja kwa maofisa kilimo, ambapo watapata taarifa kuanzia hatua ya kuotesha mmea shambani mpaka hatua ya mavuno jambo ambalo litaongeza ufanisi wa kazi  na kupata takwimu sahihi za uzalishaji nchini,” amesema.

Amesema mapema Novemba mwaka huu wamefanya mkutano na maofisa kilimo wa mikoa 24 nchini, lengo ni kuwapatia elimu namna ya matumizi ya teknolojia hiyo kukusanya taarifa za uzalishaji wa mazao mbalimbali ya kimkakati.

“Teknolojia hii ni mpya nchini itakuwa msaada wa kupata taarifa za maeneo yote yanayolimwa mazao hata maeneo yasiyofikika kwa urahisi jambo litakalisaidia nchi kufunguka katika sekta ya kilimo,” amesema.

Mlowe amesema pia itasaidia Taifa kujua kiwango cha uzalishaji kwa mwaka husika, tofauti na mfumo wa zamani ambao maofisa kilimo walikuwa wakikadiria takwimu kutokana na kushindwa kufika baadhi ya maeneo.

Kwa upande wake, Ofisa Kilimo Wilaya ya Rungwe, Juma Mzara amesema kuwa kukua kwa teknolojia kutaleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya kilimo, ikiwamo kuvuka malengo ya uzalishaji

Naye, mkulima Witness Kamwela amesema mfumo huo pia utakuwa mkombozi mkubwa na kuchochea uwekezaji wa kilimo chenye tija kubwa kwa Taifa.