Ulikuwa mwaka wa corona, uchaguzi na sasa Krismasi

New Content Item (1)
Ulikuwa mwaka wa corona, uchaguzi na sasa Krismasi

Muktasari:

Krismasi imekosa mvuto mno. Ni kama Januari imefika tayari. Watu mifuko yao imejenga undugu na maeneo kama ya Same. Kwa wenyeji wa huko watakuwa wameelewa, ni eneo kame sana. Watu hatuna kitu lakini madukani vitu vimejaa. Kuanzia Kariakoo mpaka Buza kule kwa Mpalange. Tatizo ukame wa faranga.

Krismasi imekosa mvuto mno. Ni kama Januari imefika tayari. Watu mifuko yao imejenga undugu na maeneo kama ya Same. Kwa wenyeji wa huko watakuwa wameelewa, ni eneo kame sana. Watu hatuna kitu lakini madukani vitu vimejaa. Kuanzia Kariakoo mpaka Buza kule kwa Mpalange. Tatizo ukame wa faranga.

Kuna vitu vinatufariji na kutusogezea siku za kuishi. La sivyo wengi tungekuwa wenyeji wa ahera kwa kujitanguliza au kutangulizwa na msongo wa mawazo na akili. Wenye ajira na wasio na ajira wote laini moja, hatuchekani. Kila uingizacho kinaishia kulipa madeni na kuvimbisha tumbo. Hatuna kipato cha ziada.

New Content Item (1)
Ulikuwa mwaka wa corona, uchaguzi na sasa Krismasi

Mwaka ulianza Januari, Februari hadi Machi. Baada ya hapo ikawa corona, uchaguzi kisha Krismasi. Ndo hivyo. Wale wa mwaka huu lazima nitoboe watakuwa wanatazamana kama mazuzu. Wabunge wa upinzani kibao hawajatoboa itakuwa we kapuku huko uswahilini Unayewaza kutoboa kwa kubeti?

Kwa wenyeji wa Dar na miji mingine mikubwa, kuna vitu vingi vya kuondoa mawazo vichwani mwetu. Hapa Dar moja ya vivutio, ni pamoja na upandaji bodaboda kwa kina dada. Unajikuta katikati ya lindi la mawazo mazito ya maisha. Huna hili wala lile. Huoni mbele wala nyuma.

Kila unachowaza unajipa jibu kuwa ni vigumu kuwezekana. Unawaza utakula nini na utafikaje kesho. Unaelekea kukata tamaa kabisa, mara ghafla bodaboda inapita mbele yako ikiwa imebeba pisi kali. Mkao wa hiyo pisi unakugeuza kutoka kwenye lindi la mawazo mpaka kwenye lindi la matamanio.

Mawazo ya njaanjaa zako yote yanakata ghafla. Unabaki kukenuakenua meno kama punguani. Unaangalia ufundi wa uumbaji wa Mungu baba Mwenyezi. Kwa viumbe hawa uzao wa Delila, Eva, Gigy Money, Nandy kama siyo Halima Mdee. Pisi zinavutia kwenye bodaboda kuliko mshahara wa kibunge. Ogopa.

Nilienda Nairobi ‘lasti yia’ kwa ‘Krismasi sizoni’. Niliona usafiri wa bodaboda namna unavyotumiwa bila ‘mekanizimu’ ya kutosha kwa virutubisho vya nafsi. Kwa pale Nairobi ukipita mitaani ukaona manzi kwa bodaboda, utadhani punda wamebeba mizigo wanapita katikati ya jiji. Hamna kitu.

Hawako ‘romantiki’ kabisa na usafiri wa bodaboda. Wanapanda kama vile wapo kusugua miguu kwenye mawe. Endapo wao ndo wangekuwa waanzilishi wa usafiri huu, bila shaka ungekosa soko kabisa. Kuna haja ya kuwapelekea semina elekezi. Ya namna ya kupanda kwa mtindo wa kurutubisha nafsi za wakware mitaani.

Lakini Daslama mjini ndo maana picha za ngono zimepungua mitaani na mitandaoni. Bodaboda zinapunguza mambo mengi zinapopakiza pisi kali. Ukiwaona kwa bodaboda unaweza kudhani wimbo wa Harmonize ule wa ‘Welcome to my bed room’. Wanajibinua kama wanaanika mbaazi. Huvutia kuliko ajira ya BoT.

Lakini pia kuna vikero hapa mjini. Na hii itasaidia sana kwa wageni hasa kutoka mikoani. Ambao wameingia ‘tauni’ kuja kula sikukuu na zaidi kushangaa zile ‘flaiova’ na mabarabara makali kila kona.

Na wengi wa mikoani wakija hupenda kupanda mabasi ya mwendokasi. Sasa lazima wajue kero ya usafiri huu. Kifupi mwendokasi vituo vyote unaweza kugeuza na basi hilo hilo. Au unaweza kuunganisha basi lingine kwa tiketi ile ile isipokuwa kituo cha Kimara tu.

Kimara ukishuka ndo basi labda ukakate tiketi nyingine upya. Miundombinu ya kituo cha Kimara ni kutoka jumlajumla au kuingia mazima.

Kama ulidhani ukubwa wa mabasi yale na ubora wa vituo vyake vikawa sababu ya uungwana na ustaarabu, imekula kwako. Unaweza ukawa wa kwanza kupanda ndani ya basi na ukakosa siti.

Na wakati mwingine ukawa umeshafika kwenye kiti, ukitaka kukaa unajikuta unakalia mtu.

Kuna kitu kilikuwa kinafanya watu wapande tu mwendokasi au kuzunguka nayo. Nacho ni ile sauti ya mwanadada anayetaja majina ya vituo. Sauti flan ‘amazing’ sana mpaka watu walikuwa wanajiuliza anatangaza kituo gani cha redio? Hivi sasa zile spika zimeisha betri, hasikiki tena yule mrembo.

Kama utakuwa umetoka zako mikoani, uliza mtu Msimbazi ndo wapi kabla ya kupanda mwendokasi. Wasimamizi wa kituo cha Msimbazi ni wanoko kuliko walimu wa nidhamu pale Jitegemee na Makongo. Wanakagua titeki kama vile ukipanda unaenda mbinguni moja kwa moja na kusamehewa dhambi zako.

Zamani abiria wa mabasi ya Mwenge-Posta kupita daraja la Selanda walikuwa wajivuni wenye kujiona bora zaidi ya abiria wa maeneo mengine. Ungedhani pengine basi za kupitia huko na abiria wake ni wateule wa Mungu. Sasa kwa mwendokasi abiria wanaojisikia sana na kujidaidai ni wanaoshukia DIT.

Kwanza hawajui kutoa sauti ya kuomba usogee au apite. Pili wakikugonga wao hawana neno samahani. Kidogo neno ‘sore’. Nalo huwatoka kwa kujilazimisha tu. Wanajikutaga sijui kina nani vile. Halafu wengi wako ‘fildi’ kwenye maofisi mbalimbali siyo waajiriwa. Ujivuni wao sijui wa nini.

Kama unatokea kule Kanda Maalumu. Uwe makini na abiria wa kituo hiki hasa wanaoshuka asubuhi, unaweza kwenda jela kwa kuua bila kukusudia kutokana na ujivuni wao. Na kama umesimama kwenye basi za kwenda Kimara, ujue kabisa utapata siti Korogweeee.

Korogwe watu wengi wanashukia pale kwa sababu kuu mbili. Wanaoelekea maeneo mengine hushuka pale ili wachukue bajaji au bodaboda. Na uvivu wa kupanda juu darajani pale Kimara mwisho. Sababu nyingine kubwa kutokana na jamii ya wakazi wa huko, Korogwe kuna baa nyingi na zote zinauza kitimoto.

Mwendokasi ndo usafiri unaopakia watu wa aina tofauti na akili mbalimbali. Utashangaa mtu anagombania siti kwa nguvu pale kituo cha Msimbazi, halafu anashukia Fire. Mwingine anagombea kwa nguvu zote wakati wa kupanda, utashangaa akiwa ndani ndo anakuuliza hii basi ya kwenda wapi?

Sijajua kwa sababu gani. Au ni aina ya mazingira yake au vipi. Ila ukweli abiria wastaarabu ni wale wa Muhimbili. Wao wanasalimia kila mtu. Hawabishani wala hawagombei wakati wa kupanda. Pia wana kawaida ya kumshukuru dereva wanaposhuka. Utasikia ubarikiwe sana dereva. Utadhani wamepanda bure.

Fujo zipo Kimara. Ndo maana kituo kikuu cha Gerezani kuelekea Kimara au wale wa Kimara kwenda mjini. Hupangishwa foleni ya kupanda kama watoto wa shule. Tena abiria wa Kimara wapo tayari wapandie gari Ubungo. Waende nalo na kugeuza nalo gerezani ilimradi tu wakae kwenye siti.

Kituo ambacho hakina mzuka na abiria hawashuki wala kupanda. Zaidi ya ‘stafu’ wa mabasi yenyewe, ni Jangwani. Kituo kimepooza kama uji wa mgonjwa. Sitashangaa nikisikia kuna kiongozi wa kiroho kapakodisha kwa ajili ya mahubiri kama Tanganyika Packers. Au mtu akodishe ageuze kama kibandaumiza.

Any way. ‘Krismasi’ inaendelea hata kama mifuko imekauka kama mabua ya kiangazi. Tuendelee kujipukutisha na kidogo tulichonacho tukisubiri ‘stresi’ za Njaanuari. Nguvu tunayotumia kustarehe ndani ya sikukuu hizi, ndo chanzo cha kilio cha Januari. ‘Meri Krismasi’.

Na Dk Levy  Ndani ya Boksi