Ulinzi umeimarishwa Mahakama ya Kisutu

Ulinzi umeimarishwa Mahakama ya Kisutu

Muktasari:

  •  Ulinzi umeimarishwa katika Mahakaman ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati leo Agosti 5, 2021 kesi ya Uhujumu Uchumi namba 63/2021 inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu itakapoitwa.



Dar es Salaam. Ulinzi umeimarishwa katika Mahakaman ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati leo Agosti 5, 2021 kesi ya Uhujumu Uchumi namba 63/2021 inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu itakapoitwa.

Mbowe anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kula njama za kutenda kosa na kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili shughuli za Ugaidi, huku wenzake watatu wao wakikabiliwa na mashtaka saba.

Mbowe alifikishwa mahakamani hapo, Julai 26, 2021 na kusomewa mashtaka yake, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Soma zaidi hapa: Freeman Mbowe aja kivingine

Nje ya Mahakaka ya Kisutu, defender moja la polisi limepaki likiwa na askari kadhaa, huku wengine wakizunguka zunguka ndani na nje ya Mahakama.

Mbali na askari hao, pia yupo Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Murilo, katika viunga vya mahakama aliongoza kikosi cha Jeshi hilo kuhakikisha ulinzi unaimarishwa.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Halfan Hassan, Adam Kasekwa maarufu kama Adamo na Mohamed Lingwenya.

Baadhi ya wanachama wa Chadema wamejitokeza mahakamani hapo.