UN yahofia uchumi, maisha Afghanistan

UN yahofia uchumi, maisha Afghanistan

Muktasari:

  • Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa Aghanistan wako kwenye kusambaratika na kuingia kwenye umaskini wa kutupwa kama jumuiya za kimataifa hazitaingilia kati na kufanya fedha kuingia nchini humo.

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa Aghanistan wako kwenye kusambaratika na kuingia kwenye umaskini wa kutupwa kama jumuiya za kimataifa hazitaingilia kati na kufanya fedha kuingia nchini humo.

Nchi hiyo hivi sasa iko chini ya utawala wa wanamgambo wa Taliban walioingia madarakani baada ya majeshi ya Marekani na washirika wake kuondoka baada ya kukaa miaka 20.

Taarifa iliyotolewa na Programu ya Maendeleo ya Umoja huo, juzi inaonyesha kuwa asilimia 97 ya Waafghanistani watatopea kwenye dimbwi la umaskini kama matatizo ya kisiasa na kiuchumi hayatatatuliwa haraka.

Taarifa mbalimbali zinasema karibu dola bilioni 10 za Benki kuu ya Afghanistan zimezuiwa nje ya nchi ambazo kama utawala wa sasa utafanya kazi vizuri zinaweza zikaachiwa na kuchochea shughuli mbalimbali nchini humo.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya Afghanistan, Deborah Lyons aliliambia Baraza la Usalama kuwa ni lazima ipatikane njia ya kuingiza fedha nchini humo ili kuzuia kuparaganyika kwa uchumi ambao pia utasababisha mtikisiko mkubwa katika jamii.

“Kuzuia kuvunjika kabisa kwa uchumi na utulivu wa kijamii,” akibainisha kuwa Afghanistan inakabiliwa na dhoruba ya migogoro.

Kutokana na hali kutotulia nchini humo na baadhi ya watu kukimbia wakihofia usalama wao baada ya Taliban kuchukua uongozi, kumekuwa na kupanda kwa bei za chakula, mafuta na benki binafsi kukosa fedha.

Taarifa zaidi zinadai kuwa mamlaka mbalimbali nchini humo zimeeleza kutokuwa na fedha za kulipa mishahara na stahiki za wafanyakazi wake

“Ni lazima uchumi uachwe upumue kwa miezi michache kwa kuupa muda utawala wa Taliban kuonyesha utawala wa hivi sasa ni tofauti na ule ulioondolewa madarakani miaka 20 iliyopita.

“Ni lazima waonyeshe walivyo tayari kuheshimu haki za binadamu, utawala bora na kupambana na ugaidi ambao umekuwa tishio duniani,” Lyons aliwaambia wanachama 15 wa baraza hilo huku akiweka wazi kuwa ni lazima wahakikishe kuwa fedha hazitumiwi hovyo.

Wafadhili wa kigeni wakiongozwa na Marekani walitoa zaidi ya asilimia 75 ya matumizi ya umma kwa Serikali ya Afghanistan ambayo hata hivyo iliondolewa madarakani na Taliban mwezi uliopita mara baada ya Marekani kuondoa wanajeshi wake walioingia nchini humo mwaka 2001 kwa lengo la kupambana na ugaidi na waliokuwa wakiwafadhili.

Utawala wa Rais wa Marekani, Joe Biden umeshaweka wazi kuwa uko tayari kuchangia misaada ya kibinadamu, lakini masuala yanayohusu uchumi na kuziachia mali za benki kuu kutategemeana na matendo ya utawala wa Taliban, ikiwemo kuwaruhusu kwa usalama raia wanaotaka kuondoka nchini humo.

Hata hivyo, Taliban tayari wameruhusu ndege za kiraia kuondoka katika uwanja wa ndege wa Kabul ambapo ndege iliyobeba abiria zaidi ya 100 ilitua Qatar juzi.

Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF), nao umezuia utawala wa Taliban kutumia Dola za Marekani milioni 440 katika huduma za dharura.

“Utawala wa Taliban unatafuta uhalali na uungwaji mkono na jumuiya za kimataifa, ujumbe wetu kwao ni rahisi kabisa. Matendo yao ndiyo yatakayotufanya sisi tuwaunge mkono,” alisema ofisa wa masuala ya diplomasia wa Marekani, Jeffrey DeLaurentis wakati wakiwaambia wajumbe wa baraza la usalama.

Urusi na China ambazo zimetangaza utayari wao wa kutoa misaada ya dharura kwa Afghanistan zimetoa wito wa kuachiwa kwa mali za nchi hiyo zilizozuiwa katika mataifa mbalimbali ili ziwasaidie Waafghanistan kukabiliana na hali ngumu ya maisha.

“Hizo mali ni za Afghanistan na lazima zitumiwe na Waafghanistan wenyewe bila vikwazo au vitisho kutoka kwa mtu yeyote.”