Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ushuhuda kibano cha kikosi kazi

Muktasari:

 Uamuzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuacha matumizi ya kikosi kazi (task force) kukusanya kodi kwa mabavu umewaibua wafanyabiashara, wakieleza madhila waliyokumbana nayo huku wakisema wako tayari kulipa kodi kwa hiari isipokuwa ziwe za haki.

  


Arusha/Moshi. Uamuzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuacha matumizi ya kikosi kazi (task force) kukusanya kodi kwa mabavu umewaibua wafanyabiashara, wakieleza madhila waliyokumbana nayo huku wakisema wako tayari kulipa kodi kwa hiari isipokuwa ziwe za haki.

Wafanyabiashara hao wamesema kwa sasa wanasubiri kurejeshewa mabilioni yao ya shilingi wanayodai yalichukuliwa na kikosi kazi.

Juzi wenyekiti wa Bodi ya TRA, Uledi Mussa alisema mamlaka hiyo imeachana na matumizi ya mabavu kwa kutumia kikosi kazi kukusanya kodi kwa kuwa hayana afya, badala yake sasa inakaa na wafanyabiashara kujadiliana nao ili walipe kodi kwa hiari.

Pia mamlaka hiyo ilisema imeondoa baadhi ya kesi mahakamani na kwenye mamlaka za rufaa, huku ikikutana na wafanyabiashara waliokumbana na misukosuko ya kikosi kazi kurekebisha sintofahamu zilizokuwepo katika maeneo mbalimbali nchini.

Kilimanjaro na Arusha ni miongoni mwa mikoa ambayo baadhi ya wafanyabiashara wake waliteswa na kikosi kazi chini ya mtutu wa bunduki, kutishwa na wakati mwingine akaunti zao kufungwa na pesa kuchukuliwa.

Tukio linalodaiwa kutikisa wengi ni la mwaka 2018, ambapo maduka ya kubadilisha fedha yalivamiwa na kikosi kazi na fedha, vifaa na hati za umiliki mali vikichukuliwa.

Suala la maduka hayo limekuwa likihojiwa bungeni mara kwa mara na miongoni mwa waliopaza sauti hizo ni Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo na mwenzake wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo.


Madhila makubwa

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tato), Wilbard Chambulo alisema yeye pamoja na wanachama wenzake, wakiwemo wamiliki wa maduka ya kubadilisha fedha, walipata madhila makubwa yaliyotokana na kikosi kazi.

Chambulo alisema yeye binafsi alipoteza zaidi ya Sh3.5 bilioni zilizochukuliwa kwenye akaunti yake na kwenye maduka yake ya kubadilisha fedha.

“Walikwenda kwenye maduka wakachukua fedha, baadaye kwenye akaunti zangu wakachukua bila kufuata utaratibu, lakini tunashukuru sana Rais Samia Suluhu amesikia kilio chetu na kuahidi kwamba tutarejeshewa,” alisema.

Alisema wanashukuru TRA kwa ushirikiano mkubwa ambao wanaendelea kupewa, ikiwemo kupitia mahesabu ya taasisi zao kuona kiasi cha kodi cha haki ambacho kinapaswa kulipwa.

“Tumefanya vikao na wakaguzi wa hesabu Dar es Salaam, Mwanza na kwa kiasi kikubwa tunashukuru TRA na maofisa kwa kuona kulikuwa na uonevu na wameahidi kuturejeshea fedha zetu,” alisema.

Alisema tayari TRA iliomba akaunti namba ili kuanza mchakato wa kurejesha fedha zilizochukuliwa na wana imani kutokana na maagizo ya Rais Samia fedha zitarejeshwa.

“Kipindi kile ilikuwa huwezi kufanya chochote, kama wakikukuta huna fedha walikuwa wako tayari hata kuuza mali zako, walituumiza sana,” alisema.

Chambulo alisema kwa sasa wafanyabiashara wengi katika sekta ya utalii na maduka ya kubadilisha fedha wanalipa kodi zao kwa hiari kutokana na utaratibu mzuri wa TRA.

“Kwa Arusha kikosi kazi kilichukuwa fedha nyingi sana na tatizo huwezi kuwa na jumla yake kwani kila mfanyabiashara alifuatwa kwa muda wake na akaunti kufungwa,” alisema.

Mfanyabiashara mwingine wa duka la kubadilisha fedha, ambaye aliomba kuhifadhiwa jina, alisema kikosi kazi kilichukua zaidi ya Sh200 milioni katika maduka yake na nyaraka zote kiliondoka nazo.

“Ilikuwa operesheni ngumu sana, hawakutoa fursa kujieleza, wao walitaka fedha tu na wametufilisi,” alisema mfanyabiashara mwingine wa Moshi.

Alisema siku moja alikwenda benki kuangalia salio akashangaa kukuta inaandika ‘00’ na ikabidi aende kumuuliza meneja kulikoni.

“Meneja akaniambia nina matatizo na Serikali, nikajiuliza matatizo gani, maana sidaiwi kodi na wala sina madai yoyote ya kodi, lakini nikaambiwa nadaiwa na wakaanza kuchota pesa, mara Sh500 milioni, mara Sh600 milioni,” alidai mfanyabiashara huyo.

Mmoja wa marafiki wa karibu wa mfanyabiashara mwingine ambaye sasa ni marehemu, alisema rafiki yake aliletewa madai ya kodi ya Sh2 bilioni ambazo hakujua zimetoka wapi na za nini na kisha kwenye akaunti yake zikachotwa Sh1.3 bilioni.

“Alikufa ghafla na inasemekana alipata presha kwa sababu alipokwenda benki akakuta wamefunga akaunti na wamechukua Sh1.3 bilioni. Ndio hivyo, haikuchukua muda akafa,” alidai.


‘Tumepokea kwa furaha’

Walter Maeda, mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), Mkoa wa Arusha, alisema yeye na wanachama wenzake wamepokea kwa furaha taarifa ya kuondolewa kwa kikosi kazi cha TRA na wapo tayari kulipa kodi za haki.

“Tumepokea taarifa vizuri sana na tunaomba pia ushirikiano wakati wa kukusanya kodi uwe wa kiungwana. Tusiwe tena tunabughudhiana, tunatishwa kwamba akaunti zitafungwa. Sasa hivi tufanye kazi kwa hekima na busara,” alisema.

“Wakusanye kodi kwa weledi na sisi tuko tayari kulipa kodi bila matatizo, ila kodi ambayo ni haki lakini sio kodi za kubambikiwa. Yaani unabambikiwa kodi hadi ufanye majadiliano sijui mpaka ifike wapi, sisi hiyo ndio hatutaki,” alisisitiza.

“Kitu kingine waangalie biashara zetu, hivi kweli inastahili kodi hii tuliyowakadiria?” alisema Maeda.

“Sio wanaangalia jengo, oooh mbona hili jengo kubwa namna hii, wanaandika tu wanavyotaka. Au mbona huyu ana magari mengi namna hii labda yanaingiza hela nyingi. Yanaingizaje hela nyingi? Njooni mkaangalie uhalisia,” aliongeza.

Mkurugenzi mmoja wa kampuni ya utalii mkoani Arusha, alisema, baada ya kikosi kazi hicho kuvamia ofisini kwake walilazimisha kupewa fedha na wakachukua hati za kusafiria za baadhi ya wafanyakazi.

“Walichukua fedha nyingi zaidi ya dola 100,000 (zaidi ya Sh230 milioni) na hadi sasa hakuna mrejesho juu ya fedha hizo,” alisema.