Utata watanda KKKT Kijitonyama, waumini moto

Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kijitonyama Eliona Kimaro.

Dar es Salaam. Utata umeibuka katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) baada ya Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP) kumpa likizo ya siku 60 Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kijitonyama, Dk Eliona Kimaro.

Pia, Dayosisi hiyo imemtaka mchungaji huyo kuripoti makao makuu ya Dayosisi Machi 17 mwaka huu atakapomaliza likizo yake.

Uamuzi huo umeibua maswali na mijadala lukuki mitandaoni na ndani ya usharika kuanzia juzi usiku na jana hali ilipamba moto baada ya waamini kufikia uamuzi wa kuanzisha makundi ya WhatsApp kupinga hatua hiyo.

Mbali na makundi hayo, mjadala kuhusu sakata hilo uliteka mitandao ya kijamii ukielezwa kwa namna tofauti, baadhi wakikosoa uamuzi huo wengine wakisema ni jambo la kawaida mchungaji kuhamishwa.

Mchungaji huyo maarufu ndani na nje ya dayosisi hiyo kutokana na mafundisho yake ambayo yamekuwa yakifuatiliwa na watu wa ndani na nje ya dhehebu hilo, alitangaza uamuzi huo Jumapili kwenye ibada.

Baadhi ya waamini wa ushirika huo waliangua kilio alipowatangazia uamuzi uliochukuliwa na viongozi wake wa DMP inayoongozwa na Askofu Alex Malasusa na wengine walikusanyika kanisani hapo wakiwa na mabango yenye ujumbe tofauti.

Juzi Jumatatu usiku zilianza kusambaa video zinazomuonyesha Mchungaji Kimaro akiwaaga waumini wa kanisa hilo akiwaeleza amepewa likizo ya siku 60 baada ya kuitwa katika ofisi ya msaidizi wa askofu na kufanya kikao pamoja na mkuu wa jimbo.

“Mimi ni mchungaji wa Lutheran, kwa hiyo ninaheshimu kiapo changu cha

kichungaji na kuishi katika kiapo na maadili…Pia kwa neema ya Mungu kwa sababu hiyo imenilazimu kutii na kwenda kwenye hiyo likizo na baadaye kuripoti kwenye ofisi ya Askofu kama nilivyoelekezwa,” alisema Mchungaji Kimaro.

Mchungaji Kimaro alitangaza uamuzi huo siku iliyofuata, Janauri 16, ilikuwa aanze semina ya neno la Mungu kuanzia.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Mchungaji Kimaro bila kufafanua juzi aliandika, “Mbingu zikikutambulisha, hakuna mwanadamu wa kukufuta”, kauli ambayo inahusianishwa na sakata hilo.


Suala la kawaida

Suala la kuhamishwa kwa wachungaji kutoka usharika mmoja kwenda mwingine  limeelezwa na askofu mmoja wa KKKT ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe kuwa ni la kawaida.

“Kila dayosisi ina utaratibu wake. Hapo Dar es Salaam nasikia hata wakuu wa majimbo wanahamishwa,” alisema.


Makundi ya Whatsapp

Mara tu baada ya video za kanisani kusambaa wafuasi wake walitumia hashtag #BringbackMchungaji ElionaKimaro kutengeneza kundi na lilipojaa wakaunda la pili.

Makundi hayo yenye watu zaidi ya 1,000 yalianzishwa kujadili suala hilo na jana asubuhi walikubaliana ikifika saa 11:30 jioni wakutane katika usharika wa Kijitonyama.

Baadhi ya wajumbe wa makundi hayo walijiandikisha kwa ajili ya kuwa na tisheti zenye ujumbe #BringbackKimaro.

Zaidi ya waamini 100 waliandikisha majina na kutuma fedha kwa ajili ya tisheti hizo walizosema zitavaliwa Jumapili na kuendelea.


Wakusanyika kanisani

Mwananchi lililokuwa limeweka kambi kanisani hapo kuanzia asubuhi, ilipofika saa 10 jioni walianza kuingia waumini kisha wakaanza kuandika mabango yenye jumbe kadhaa na kuimba nyimbo mbalimbali.

Ilipofika saa 12:00 jioni, kengele iligongwa kwa ajili ya ibada ya jioni na waamini hao, wengi wao wakiwa wanawake, walisimama na mabango na kuanza kuimba.

Miongoni mwa nyimbo ni pamoja na tuna imani na Dk Kimaro na tunamtaka mchungaji wetu huku wakilizunguka kanisa hilo.

Baadhi ya mabango yalikuwa na ujumbe; “mimi ni wa mbao”, “upendo ni wa gharama”, “vita ipo mwilini”, “Askofu Dk Alex Malasusa staafu kwa heshima.”

Friday Jones ambaye ni muumini wa kanisa hilo alisema Mchungaji KImaro

ametoka likizo mwezi Desemba hivyo hawaoni sababu ya kupewa likizo

nyingine ya miezi miwili.

"Mafundisho yake yametutoa mbali, watu wengi wamekuwa wakifuatilia na kupokea mafundisho yake. Tunataka mchungaji wetu arudi mafundisho yake yametusaidia ukiacha uchungaji amekuwa na roho ya kipekee ya kusaidia watu,” alisema Jones.

Muumini mwingine, Enea Mwantika alisema Mchungaji huyo alikuwa ameanza semina ya wiki mbili lakini ghafla amepewa barua ya likizo, jambo hilo limewaumiza sana.

"Hapa kuna mtu amehusika, sisi ndio tunayemfahamu mafundisho yake wapi yanatupeleka na  nini tunachokipata, haiwezekani mumpe likizo mtu aliyetoka likizo," alisema Mwantika.

Juhudi za Mwananchi kuupata uongozi wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani akiwemo Askofu Malasusa ziligonga mwamba baada ya kuelezwa kuwa askofu huyo yuko nje ya nchi na simu yake ya mkononi ilipopigwa kwa njia ya WhatsApp iliita na haikupokelewa. Hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi hakujibiwa.

Katibu Mkuu wa KKKT Robert Kitundu alipotafutwa alisema suala hilo lipo chini ya Dayosisi husika na kuwa suala hilo halijafikishwa rasmi makao makuu.

“Kanisa la Kiinjili la Kilutheri lina dayosisi nyingi kunapokuwa na dayosisi maana yake kunakuwa na askofu ambaye anamiliki lile eneo, mimi kama Katibu Mkuu wa Kanisa, labda nimeambiwa au vinginevyo kwa sasa wazungumzaji ni Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ambaye ni Alex Malasusa au Katibu wake,” alisema Kitundu.

Mwananchi lilifika katika ofisi kuu za jimbo hilo Azania Front na

baada ya kumuulizia Askofu Malasusa lilielezwa amesafiri kikazi

nje ya nchi.

Hata hivyo, Katibu wa Dayosisi hiyo, Goodluck Nkini alikubali kuzungumza na mwandishi na kuomba awahudumie wageni wengine watatu waliotangulia.

Baada ya muda wa saa 1 na dakika 45, msaidizi alimweleza mwandishi Katibu asingeweza kuzungumza kwa kuwa masuala hayo ni ya kichungaji taaluma ambayo yeye hana.

Mwananchi ilimtafuta msaidizi wa Askofu, Chediel Lwiza ambaye alihusika kukaa kikao na Dk Kimaro na kabla ya kuulizwa kuhusu sakata hilo alikata simu mara baada ya mwandishi kujitambulisha.


Hali ilivyokuwa mitandaoni

Huko mitandaoni mijadala ilikuwa ya kila aina na kila mmoja akizungumza lake. Si viongozi wa kidini waliolizungumzia hilo wao pekee bali wanasiasa na makundi mbalimbali kila mmoja akizungumza kwa mtazamo wake.

Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza katika andiko lake aliloliweka kwenye facebook yake na baadaye kusambaa kwa kasi mitandoni alilipa jina la ‘somo la kemia kanisani. Wivu + Tamaa X Ujinga wa mamlaka= burudani mitandaoni.’

Dk Bagonza alisema,”kuna watu wamepigwa na kuumizwa, wasizuiwe kulia. Kuna watu hawajui chanzo, wasizuiwe kuhoji hoji. Kuna watu wanaujua ukweli wote; mitandao si mahali pa kuusemea.”

“Kuna watu wamekosea njia; wametibu dalili badala ya ugonjwa. Ni wakati wa kujifunza-si kufafanua wala kujitetea. Kuna watu wanataka huruma; ni haki kuhurumiwa ukiumizwa lakini huruma ya binadamu haitoshi na haiponyi,” alisema

“Kuna watu wanashangilia. Ni sawa na ngedere wachanga wachekao msitu unaoteketea wasijue jioni watalala wapi. Shoka lipo shinani…tunaona nini?


Mti mbichi? Mkavu utakuwaje?

“Mchungaji apigwaye ili kutawanya kondoo?, ng’ombe aliyevunjwa mguu ili arejee zizini?, Mfalme katili anayefukuza giza kwa kuzima mshumaa?, mtoto mkaidi asiyefaidi mpaka siku ya Idd?, baba mjinga anayekerwa na nyota ya jirani kuliko giza la nyumbani kwake?

Mwisho Askofu Bagonza akasema, “kuna kitu hakiko sawa mahali. Tunahubiria wengine maridhiano. Sasa turidhiane sisi."

Naye aliyekuwa Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, aliweka picha ya Dk Kimaro kwenye Twitter yake na kuandika,“Poleni sana waumini wote KKKT Kijitonyama, Mchungaji Eliona Kimaro hakuwa wa Kijitonyama peke yake, wapagani na madhehebu mengine tulibarikiwa sana na mahubiri yake. Natarajia kumuona Kimaro madhabahuni tena, popote pale.”

Kwa upande wake, Askofu Mkuu Emmaus Mwamakula, Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania & Afrika Mashariki alindika andiko ambalo nalo kama la Askofu Bagonza lilizunguka kwa kasi mitandaoni.

Askofu Mwamakula alisema Dk Kimaro ni miongoni mwa watu maarufu, hivyo suala hili haliwezi kuchukuliwa wepesi.

“Hapa tumeweka mtazamo wetu wa kitheologia ili kutoa mchango wetu katika hoja hii. Ni dhahiri kuwa misimamo binafsi ya Dk Kimaro imemtia katika misuguano mingi na uongozi wa KKKT kwa kipindi kirefu. Lakini, misimamo hiyo iliweza kuvumiliwa ndani ya KKKT na ndio maana alipewa kuongoza Usharika mkubwa katika Dayosisi ya Mashariki na Pwani,” alisema Mwamakula.

Aidha, Askofu huyo alizungumzia masuala mbalimbali aliyodai yamekiukwa na Dk Kimaro ambayo viongozi wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani wasingeweza kuyafumbia macho ikiwemo la matamshi ya Dk Kimaro aliyoyatoa hivi karibuni baada ya kutoka Marekani ndiyo yaliyopelekea uongozi kumuita na kumpa likizo.

“Kwa mujibu wa video iliyosambaa, Dk Kimaro amesikika akisema vijana wa Kikristo sio waaminifu bali vijana wa Kiislamu ndio waaminifu kuliko vijana wa Kikristo.

“…amesikika pia akisema watu wote wanaosimama madhabahuni (Wainjilisti, Wachungaji na Maaskofu] ni matapeli na watu wote waliokaa kwenye viti [vya ibadani - Wazee wa Kanisa na waumini) ni matapeli pia. Mch. Dkt. Kimaro amekwenda mbali zaidi na kusema takwimu [hajataja ni takwimu gani na taasisi iliyotoa takwimu hizo] zinaeleza hayo aliyosema.”

Askofu Mwamakula aliwaomba waamini kuwa watulivu wakati suala hilo linashughulikiwa.