Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uzalishaji madini ya kinywe kuanza karibuni Ruangwa

Msimamizi wa mradi wa kuchimba na  kuchakata madini ya Kinywe kutoka kampuni ya Lindi Jumbo, Mhandisi Chediel Mshana akimuelekeza jambo Waziri wa Madini, Antony Mavunde (wa pili kulia). Picha na Bahati Mwatesa

Muktasari:

  • Mradi huo utakapoanza Machi 2024 unatarajiwa kuzalisha tani 40 za madini hayo kwa mwaka na kuongeza nafasi za ajira

Ruangwa. Uzalishaji wa madini aina ya kinywe unatarajiwa kuanza Machi 2024 baada ya kukamilika kwa mgodi unaojengwa wilayani Ruangwa Mkoa wa Lindi.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Desemba 28, 2023 na meneja msimamizi wa mradi wa kampuni ya Lindi Jumbo, Chediel Mshana inayohusika na ujenzi wa mgodi huo, wakati akitoa taarifa kwa Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.

“Hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 90 na kufikia Machi 2024 utaanza uzalishaji na tunatarajia kuwa utazalisha tani 40 kwa mwaka.

"Tunaiomba Serikali itusaidie kutupatia umeme, ili tutakapoanza uzalishaji mradi usipate changamoto ya umeme kama ilivyo sasa,”amesema Mshana.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema mgodi huo ukikamilika mapema utakuwa na tija katika sekta ya madini.

“Huu utakuwa kati ya miradi michache mipya ya uchimbaji wa madini mkakati ya kinywe nchini Tanzania. Ni dhamira ya Serikali kuona shughuli za uchimbaji wa madini zinaongezeka, ili kuchochea ukuaji wa sekta ya madini na kuleta matokeo chanya kwenye uchumi wa nchi na kuongeza nafasi za ajira,”amesema Waziri Mavunde.

Aidha, Waziri Mavunde amewataka wamiliki we ye leseni za madini nchini kuziendeleza kwa mujibu wa sheria inavyoelekeza, kwani zipo nyingi hazifanyiwi kazi na hivyo kuzorotesha ukuaji wa sekta ya madini.

“Nitumie fursa hii kuwatangazia wale wamiliki wa leseni wasiondeleza maeneo yao kuzingatia matakwa ya sheria juu ya umiliki wao wa leseni husika, vinginevyo leseni hizo zitafutwa kwa mujibu wa sheria na kutoa nafasi ya watu wanaoweza kuendeleza,”amesema Mavunde.

Mkuu wa Wilaya wa Ruangwa, Hassan Ngoma amesema kukamilika kwa mradi huo kutachochea ukuaji wa sekta ya madini na maendeleo katika wilaya hiyo, huku akiomba huduma ya umeme ifike katika kijiji ambacho mradi huo unatekelezwa.

"Ni kweli changamoto ya umeme ipo, waziri tunakuomba utusaidie kutufikishia changamoto hii ili watutatulie pindi uzalishaji utakapoanza, kusiwe na changamoto tena ya umeme,"amesema Ngoma.

Salma Juma, mkazi wa kijiji cha Matambalale amesema mradi utakapokamilika utasaidia kukuza uchumi wa Ruangwa  na Lindi kwa ujumla kutokana na fursa zitakazopatikana mgodini hapo.

"Huu mradi utakapokamilika, sisi wakazi wa Ruangwa tutanufaika nao, kwani uchumi utakua na ajira zitapatikana,"amesema Salma