Uchimbaji wa madini ya Gypsum kuanza Kilwa
Muktasari:
“Halmashauri itapata ushuru kutokana na mradi wetu na pia tutalipa mrabaha kwenye Serikali kuu hivyo mradi ni mzuri kwa manufaa yetu sote,”alisema.
KAMPUNI ya Mishangu International Ltd, inatarajia kuanza uchimbaji wa madini ya kutengeneza Gypsum katika eneo la Makangaga lililopo Kilwa, baada ya kupata cheti cha tathimini mazingira kutoka Baraza la Mazingira Tanzania (NEMC).
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa cheti hicho Msemaji wa kampuni hiyo, Godbless Kweka alisema mradi wa uchimbaji wa madini hayo utaanza Februari mwakani na utaweza kufaidisha watu wa eneo husika kwa kutoa ajira.
“Tulikuwa tunasubiria hiki cheti kutoka NEMC na tumekipata baada ya kufanya tathimini ya mazingira kama yanaweza kuturuhusu kufanya mradi huo katika eneo hilo,”alisema Kweka na kuongeza;
“Tumefurahi kupata cheti hiki kwa kuwa hatungeweza kuendelea na shughuli yoyote bila kukipata ni kitu muhimu katika kufanikisha mradi wetu.”
Alisema kuwa baada ya tathimini kufanyika imeonekana wanaweza kuendelea na mradi huo na kwamba hivi sasa wanajiandaa kuanza kazi rasmi ya uchimbaji huo.
Kweka alisema mbali na mradi huo kuwanufaisha wananchi wa eneo la Makangaga pia utaliingizia taifa fedha na pia kuinufaisha kimapato Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.
“Halmashauri itapata ushuru kutokana na mradi wetu na pia tutalipa mrabaha kwenye Serikali kuu hivyo mradi ni mzuri kwa manufaa yetu sote,”alisema.
Alisema madini yatakayochimbwa katika eneo hilo yataweza kutengeneza Gypsum, sementi na gypsum powder ambazo hutumika katika maeneo mbalimbali ya ujenzi hapa nchini.