Madini ya nickel kuanza kuchimbwa Ngara

Muktasari:
- Mradi wa uchimbaji madini ya nickel ni wa miaka mingi, zaidi ya miaka 33 tangu kampuni zianze kufanya utafiti, sasa kampuni ya Tembo Nickel iko tayari kuanza uchimbaji huo baada ya kupata Baraka za mkoa.
Bukoba. Kampuni ya uchimbaji wa madini ya Tembo Nickel imepata baraka rasmi za mkoa kwa ajili ya kuanza uchimbaji wa madini ya nickel yaliyopo Ngara mkoa wa Kagera.
Madini ya nickel yanaanza kuchimbwa ikiwa ni baada ya kufanyiwa utafiti kwa kipindi cha miaka 33 na mkataba wa uchimbaji madini ulisainiwa na Hayati John Pombe Magufuli mkoani Kagera mwanzoni mwa mwaka huu na Octoba 27, Kampuni ya Tembo Nickel ilipata leseni kubwa ya uchimbaji.
Baraka hizo zimetolewa leo Novemba 11, 2021 na mkuu wa mkoa wa Kagera Meja Generali Charles Mbuge kwa niamba ya wananchi wa mkoa huo lengo likiwa ni kuiruhusu Kampuni hiyo ya uchimbaji madini ya Tembo Nickel kuanza rasmi shughuli za uchimbaji madini ya Nickel.
Mbuge amesema, mradi wa uchimbaji madini ya Tembo Nickel ni wa miaka mingi, zaidi ya miaka 33 tangu kampuni zianze kufanya utafiti na kuwa hatua ya Kampuni ya Tembo Nickel kujitambulisha kwenye mkoa ni hatua nzuri ya kuanza mara moja shughuli za uchimbaji huo.
“Januari 19, 2021 Hayati John Pombe Magufuli alitia saini ya uchimbaji madini hayo hivyo kuanza kwa uchimbaji huo kutatoa fursa kwa wananchi wa Ngara kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi pia Serikali inategemea kupata mapato mengi kupitia ushuru wa huduma (service levi),” amesema Mbuge.
Kwa upande wake, Meneja mkazi wa ya Tembo Nickel hapa nchini, Benedict Busunzu amesema kuwa, baada ya kujitambulisha kwa mkoa na kupata ruhusa rasmi ya mkuu wa Mkoa sasa Tembo Nickel iko tayari kuanza kuwashirikisha viongozi waandamizi wa mkoa pamoja na wanajamii kutoka vijiji vilivyozunguka eneo la mradi na kuanza kwa shughuli ardhini.

Meneja mkazi hapa nchini wa Kampuni ya uchimbaji madini ya Tembo Nickel Benedict Busunzu akizungumza kwenye mkutano wa kutambulisha Kampuni yao kwenye katika uongozi wa mkoa wa Kagera pamoja na kupata baraka za mkoa ili waanze rasmi uchimbaji wa madini ardhini. Picha na Alodia Dominick
Busunzu amesema serikali ya Tanzania itanufaika na kodi na katika uzalishaji wa madini itapata 16 asilimia na Tembo Nickel itapata 84 asilimia na katika mapato yatakayopatikana serikali itapata 50 asilimia na Kampuni ya Tembo Nickel itapata 50 asilimia pia.
Amesema wanatarajia kuwa, katika kipindi cha ujenzi zaidi ya ajira 1,000 kupitia wakandarasi wao zitahitajika na kipaumbele cha ajira na mafunzo itakuwa kwa wakazi wa mkoa wa Kagera na wanategemea mwaka ujao shughuli kuu zitahusisha marejeo ya upembuzi yakinifu wa uchimbaji madini kabla ya kuanza shughuli nzima ya ujenzi.