VIDEO: Kifo kingine cha raia akiwa mikononi mwa polisi

Muktasari:

  • Ndugu wa  marehemu Andrew  Kiwia dereva wa Toyota Hiace na mkazi wa Mnazi Moshi, wamesusa kuchukua mwili wa ndugu yao kwa maelezo kuwa alifia mikononi mwa polisi huku walinzi hao wa usalama wakieleza kuwa alifariki katika jaribio la kujinyonga akiwa mahabusu ya kituo kikuu cha wilaya.
  • Ndugu wanadai maiti ina jeraha kichwani

Moshi. Sakata la watuhumiwa kufia mikononi mwa polisi sasa limehamia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola baada ya familia moja mjini hapa kukataa kuchukua maiti ya ndugu yao ambaye wanadai alifia mikononi mwa walinzi hao wa usalama.

Waziri huyo amekuwa akikumbana na maswali bungeni na kwenye mikutano na waandishi wa habari kuhusu ongezeko la matukio ya watuhumiwa kufia mikononi au vituo vya polisi na hivi karibuni alijibu kuwa si kila anayefia polisi hutokana na makosa ya polisi.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi linadai mtuhumiwa huyo, Andrew Kiwia (pichani) ambaye ni dereva wa Toyota Hiace na mkazi wa Mnazi Moshi, alifariki katika jaribio la kujinyonga akiwa mahabusu ya kituo kikuu cha wilaya, maelezo ambayo familia hiyo haikubaliani nayo kwa madai kuwa maiti ina jeraha kichwani.

Wakati Polisi wakidai alifanya jaribio la kujinyonga akiwa mahabusu na walipomchukua ili kumpleka hospitali kuokoa maisha yake alifariki njiani, ndugu wanadai alifariki kutokana na kipigo cha askari.

Taarifa zinadai Andrew alikamatwa na polisi waliokuwa doria saa 5:00 asubuhi Ijumaa iliyopita akiwa mwenzake, Obasanjo Kitwi, jirani na stendi ya Kiborloni na kupelekwa kituo cha kikuu.

Vyanzo kutoka ndani ya polisi vinadai kuwa mtuhumiwa huyo na mwenzake walikamatwa wakiwa na pombe aina ya gongo, lakini ndugu wamepinga taarifa hiyo wakidai alikamatwa wakati akimnyoa nywele Obasanjo na taarifa za kifo hicho zilijulikana Jumatatu saa 3:30 asubuhi.

Hata hivyo, bado haijafahamika mtuhumiwa huyo aliwezaje kujinyonga kwa kutumia suruali yake aina ya jeans akiwa mahabusu, bila wenzake kushuhudia na kutoa taarifa kwa polisi wa zamu.

“Natamani kuonana na Waziri Lugola kuhusu suala hili,” alisema Haika Mesia Kimambo ambaye ni mama wa marehemu, alipozungumza na Mwananchi nyumbani kwake eneo la Mnazi jana.

Haika alihoji iweje mwanaye achukuliwe na polisi akiwa hai na kisha wakabidhiwe akiwa amekufa na kuhoji kama polisi pamegeuka mahali pasipo salama kwa maisha ya raia.

“Mtoto wangu hajawahi kukutwa na kesi yoyote tangu azaliwe. Naomba nikutane na huyo waziri ana kwa ana anieleze kwa nini mtoto wangu anauawa wakati hajafanya tukio lolote la kihalifu.”

Mama huyo alidai kuwa wao kama familia, hawatazika mwili wa kijana wao hadi polisi watakapoeleza kwa nini walimuua mtoto wao kinyama badala ya kumfikisha mahakamani kama alikuwa na kosa.

Taarifa za msamaria mwema

Siku hiyo, raia ambaye hakujitambulisha na ambaye alidai alikuwa kituoni, aliipigia simu Mwananchi kueleza kuwa kuna kuna mtu amekufa akiwa mahabusu kutokana na kipigo.

Mtoa taarifa huyo alidai kulikuwa na jitihada za polisi kutoa mwili wa marehemu ili ndugu ambao walikuwa kituoni hapo tangu asubuhi kufuatilia suala hilo wasiweze kujua.

Hata hivyo, polisi waliiambia Mwananchi kuwa hakuna mtuhumiwa aliyefia mahabusu, bali yuko aliyepelekwa hospitali kwa matibabu.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Koka Moita alisema kijana huyo alifanya jaribio la kujinyonga akiwa mahabusu na ndipo alipopelekwa hospitali, lakini akiwa njiani alifariki dunia.

Koka hakutaka kuingia kwa undani zaidi kuhusu tukio hilo zaidi ya kueleza kuwa polisi wameanzisha uchunguzi baada ya familia kudai wamekuta marehemu ana majeraha mwilini.

Daktari Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi, Dk Japhet Boniface alipotafutwa jana, alisema ndio ametoka chumba cha upasuaji hivyo akiwa na nafasi nzuri angemtafuta mwandishi wetu.

Lakini Mwananchi ilipofuatilia suala hilo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mawenzi, ilielezwa kuwa hakukuwa na mgonjwa kutoka kituo cha polisi.

Jana, ndugu wa marehemu walimpigia simu mmoja wa waandishi wa gazeti hili, wakisema hawatazika hadi wakutane na Waziri Lugola.

Mama wa marehemu alisema siku hiyo ya Jumatatu walikwenda kituoni hapo lakini walifukuzwa na hawakujua ni kwa sababu gani lakini baadaye waligundua ni kutokana na tukio hilo.

“Tukiwa Kituo Kikuu cha Polisi mjini Moshi tulifukuzwa na hatukujua tunafukuziwa nini, kumbe kuna gari ya polisi ililetwa kwa ajili ya kubeba mwili wa mwanangu,” alidai mama huyo.

“Baada ya sisi kufukuzwa, jirani alifuatilia na aliona mwili ukiwa umebebwa kutoka ndani ya chumba kimoja cha polisi na kuingizwa kwenye gari ya polisi ndipo mwili huo ulipelekwa Mawenzi.”

Mama huyo alidai taarifa za polisi kuwa mtoto wake alifia hospitali si za kweli kwa kuwa alitolewa polisi akiwa ameshakufa.

“Kuna kijana alikuja nyumbani ametumwa na polisi. Huyu kijana alisema ametumwa na askari aje atoe taarifa ya kifo cha mwanangu,” alidai mama huyo.

“Aliniambia kuna namba ambazo amempa kijana huyo aniletee. Alinipa zile namba nikapiga nikamwambia mimi ni mama yake na kadogoo askari yule alinijibu kuwa mtoto wenu amekufa.

“Nikamwambia unasemaje? Yule askari akanijibu hana maelezo zaidi akakata simu. Baada ya hiyo taarifa hatukuishia hapo tulienda Mawenzi kujua kama ni kweli kijana wetu alifia hospitali ama la.

“Tulizunguka kila mahali kuangalia faili lakini hatukukuta jina lake. Tulienda jengo linalohifadhia maiti tukauliza kama kijana wetu alifia pale, wahudumu wakasema maiti ililetwa na polisi.”

Kaka adai kuona kovu

Akizungumza na gazeti hili, kaka wa marehemu, Frank Kiwia alidai kuwa alipouchunguza mwili wa mdogo wake aliona paji la uso likiwa limepasuka na mikono ilikuwa na majeraha makubwa.

“Shingo yake alikua imekatwa na kitu kama katani sio suruali kama polisi wanavyodai,” alisema Frank.

“Tunataka polisi watuambie ukweli wa hilo jambo. Ni nini kilitokea kwa sababu mdogo wangu alikuwa haumwi wala si mhalifu, sasa iweje ajinyonge polisi? Huyu ndugu yetu hajawahi kuumwa ugonjwa wowote na sisi hatuwezi kuzika wakati hatujajua ukweli wa hili.”

Aliyekuwa na marehemu

Obasanjo, kijana ambaye ndugu wanadai alikuwa ananyolewa na Andrew, alidai siku hiyo walipelekwa kituoni na ilipofika saa 3:00 usiku alipata usingizi mzito na aliposhtuka hakumuona marehemu ingawa wote waliingizwa mahabusu moja.

“Nilipostuka nilimkuta hayupo sijui alipelekwa wapi. Nilifikiri ameachiliwa kwa sababu anajuana na watu wengi, lakini nilipoachiwa Jumatatu na kufika nyumbani nikaambiwa amekufa. Hadi sasa sijaamini amekufakufaje.”

Wengine waliofia vituoni

Mkoani Mbeya, ndugu wa marehemu Frank Kapange, wamesusa kuchukua mwili wake zaidi ya siku 100 sasa wakiomba Mahakama itoe amri ya kufanyika uchunguzi wa kina kuhusu kifo chake wanachodai kilisababishwa na polisi.
Frank alifariki dunia Juni 4 na mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Kanda ya Mbeya.

Aidha, Machi 25 wakazi wa Kata ya Iyela, Mbeya walizusha tafrani kubwa wakifuatilia kifo cha Allen Mapunda (22), aliyedaiwa kufariki dunia saa chache baada ya kuachiwa kutoka kituo kikuu cha polisi alikokuwa akishikiliwa

Aprili 27, Suguta Chacha (27) alifariki dunia akiwa mikononi mwa polisi na
Julai 27, mkazi wa Kijiji cha Rubambagwe, wilayani Chato, Geita, Pascal Kanyembe (39) alifariki akiwa mikononi mwa polisi baada ya kukamatwa.

Soma Zaidi: