Prime
VIDEO: Mfahamu mwanamke anayejitolea kukumbatia watoto njiti Hospitali ya Amana
Msimamo wa hospitali
Mganga mfawidhi wa Amana, Bryceson Kiwelu anasema hospitali hupokea watoto waliotupwa kutoka Jeshi la Polisi, hivyo wanakuwa hawana msaada.
“Pia, wapo wanaotelekeza watoto hapa, amejifungua salama mtoto hakutimia wanakimbia, hivyo wodi hii wameona uwe utaratibu wa kusaidia maana wanapokaa kwenye mashine pekee wanachelewa kukua,” anasema Dk Kiwelu.
Ofisa muuguzi mwandamizi wa wodi ya watoto wachanga, Reinfrida Zinga anasema kuna changamoto ya kutelekezewa watoto, hivyo wanaona kazi anayofanya Mariam inasaidia.
“Hii ni wodi ya watoto wachanga kuanzia umri wa sifuri mpaka siku 28, inafanya huduma zote kwa watoto waliozaliwa lakini hawakulia vizuri, wenye shida kidogo na waliozaliwa na uzito mdogo anaweza kuwa amekomaa na wale ambao hawakukomaa, yaani njiti.
“Njiti ndiyo tuna changamoto, endapo inatokea mama ametelekeza watoto wodini na wengine mtaani wanaletwa na maofisa polisi na wengine wanaona kazi kuwakumbatia mpaka aje afikie zile kilo zinazotakiwa wanakimbia,” anasema.
Anasema wao kama kitengo walikaa wakaona umuhimu wa kumruhusu Mariam asaidie watoto hao ili wakue kwa haraka.
Akieleza namna watoto wanavyotelekezwa anasema, “huwa inatokea wanakuja kunyonyesha, mkiona asubuhi mama hajaja njiti kabaki peke yake na saa zote anabaki mama haji, ikifika jioni mnajua wenu huyo tayari ametelekezwa.”
Anasema kabla ya kukumbatia, huhakikisha wanalinda afya ya mama na mtoto kwa kuwachukua vipimo vya maabara.
“Mariam anakumbatia mtoto ambaye hamjui kwa kangaruu, hachukui muda mrefu mtoto anakuwa ameongezeka kilo na kisha tunampa tu nauli anarudi nyumbani kwake, hatuna bajeti ya kumlipa, tunampa tu chakula siku anazokuwa hapa,” amesema.
Amesema mtoto akikamilika kuna utaratibu maalumu ambao hufanyika kupitia ofisi ya ustawi wa jamii na Jeshi la Polisi.
Ofisa huyo anasema huandaliwa kumbukumbu za mtoto na kisha hupelekwa Kituo cha Kulelea Yatima cha Msimbazi Center.
Amesema Mariam alianza kazi Aprili mwaka huu kwa kulea mtoto ambaye mama yake alifariki dunia.
Anaeleza mtoto huyo licha ya kulishwa kwa miezi minne hakuongezeka uzito, lakini ndani ya wiki moja ya kukaa kifuani mwa Mariam aliongezeka na walimpeleka Kituoni Msimbazi Center.
“Akakumbatia tena watoto wengine wawili, ambao mama zao waliwatelekeza hapa ambao nao wakaongezeka uzito haraka na wakaenda Msimbazi,” anasema.
Anasema hakuna manufaa ambayo mama huyo anayapata zaidi ni kwa mtoto. “Anajitolea, kama Serikali inaweza kumwangalia kwa namna nyingine waone watamsaidiaje maana yeye anajitolea kukumbatia mtoto ambaye si wa kwake.”
Anasema awali watoto walikuwa wanakaa kwenye mashine muda mrefu.
Faida za kangaruu
Ofisa huyo anasema kukumbatia husaidia watoto, hasa katika magonjwa ya mfumo wa kifua kwa sababu wanapata joto la mama moja kwa moja.
“Anapopata joto anakua kwa haraka na mtoto hulishwa kwa wakati, akilia mama anachukua maziwa anampa anakunywa analala anamweka kifuani, kwa hiyo anakua haraka,” anasema Zinga, akieleza kuna tofauti kubwa kati ya mashine na joto la mama.
Amesema mashine hutoa joto tu ambalo halina majimaji, lakini kangaruu kwa sababu ni ngozi kwa ngozi, hata ngozi ya mtoto huwa laini kutokana na mama kutokwa jasho.
Zinga anatoa wito kwa kinamama kwamba watoto njiti hukua wakitunzwa vizuri.
Hata hivyo anasema, “tuna vitanda sita pekee, lakini watoto waliozaliwa kabla ya wakati ni zaidi ya 20, kangaruu wanafanya sita wanaondoka wanakuja wengine sita angalau tuwe na vitanda 20 mpaka 25 tutapunguza watoto kukaa muda mrefu hospitalini,” amesema.
Amesema kukosekana kwa vitanda watoto wengi wanaishi kwenye mashine ya joto, hivyo kukua taratibu, jambo linalochangia ndugu kuchoka kuhudumia kinamama kwa muda mrefu na wengi kutelekezwa na waume na ndugu.
“Mama akitelekezwa linakuwa jukumu la ofisa uhusiano ambaye atahakikisha mama anakula na siku anaporuhusiwa anarudishwa mpaka nyumbani kwa gharama za hospitali.”
Utaratibu
Ofisa habari, mahusiano na elimu ya afya katika Hospitali ya Amana, Sara Mahena anasema hupokea watoto waliotupwa kutoka Jeshi la Polisi wakiwa na fomu namba tatu (PF3) na huwasajili ķwa ajili ya uchunguzi wa afya.
Ikibainika ana shida ya kiafya, hulazwa na vinginevyo kitengo cha ustawi wa jamii hutafuta makao ya mtoto.
Amesema iwapo akiwa mchanga na hajatimia hutunzwa kwa njia ya kangaruu.
Ofisa ustawi wa jamii Hospitali ya Amana, Sufiani Mndolwa anasema wanapoletewa mtoto husimamia matibabu.
“Akiruhusiwa tutamtafutia makao kwa kumuombea hifadhi ya muda tunapotafuta makao ya kudumu, labda familia itajitokeza wakati huo shauri lipo mahakamani. Likiisha itatoa kibali cha kumkabidhi mzazi mtoto na ikitujulisha kwamba hana msimamizi anaweza kuasiliwa,” amesema.