Vijana 5,000 wahitimu mafunzo ubunifu wa kidijitali

Muktasari:
- Mafunzo hayo yaliyodumu kwa wiki 16 yamefanyika kwa mara ya pili katika nchi tofauti za Tanzania, Kenya, Afrika Kusini, Nigeria na Zambia wanafunzi wakipata stadi za digitali zinazoweza kuuzwa kwenye soko la ajira.
Dar es Salaam. Zaidi ya wanafunzi 5,000 kutoka nchi tano za Afrika wamehitimu kozi ya ubunifu programu iliyokuwa ikiendeshwa na shirika linalojitolea kuwawezesha vijana wa Kiafrika kiteknolojia la Power Learn Project.
Mafunzo hayo yaliyodumu kwa wiki 16 yalifanyika kwa mara ya pili katika nchi tofauti za Tanzania, Kenya, Afrika Kusini, Nigeria na Zambia wanafunzi wakipata stadi za digitali zinazoweza kuuzwa kwenye soko la ajira.
Sherehe za mahafali zilizofanyika hivi karibuni zilitoa jukwaa kwa wahitimu kuonesha suluhisho zenye ubunifu kwa changamoto kubwa katika bara la Afrika, ikiwamo katika mabadiliko ya hali ya hewa, afya, na usalama wa chakula.
Akizungumza katika mahafali hayo jana Desemba Mosi, Ofisa Mkuu wa Ukuaji na Operesheni wa shirika hilo, Mumbi Ndung'u, amesema vijana hao wako katika nafasi nzuri ya kutumia stadi zao za kiufundi kutatua matatizo ya kawaida katika jamii wanazotoka na pia yanathibitisha umuhimu wa ushirikiano katika kuendesha ajenda ya maendeleo ya teknolojia kote Afrika.
"Mahafali ni zaidi ya mafanikio binafsi. Ndani ya miaka miwili tu, tumehamasisha jamii yenye nguvu ya wahitimu wanaotarajiwa kuwa viongozi wa baadaye, watetezi wa mabadiliko, na wazalendo wa dunia bora," amesema.
Mmoja wa wahitimu kutoka Tanzania Michael Msita amesema kuhitimu leo ni uthibitisho wa safari ya kushangaza waliyopitia.
PLP imeniunganisha na jumuiya ya kimataifa yenye watu wenye nia moja. Nina imani safari yangu inaanza leo, tunasherehekea siyo tu mafanikio ya mtu binafsi lakini mafanikio ya jitihada za pamoja."
Waliohududhira mahafali hayo ni pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Utawala la PLP, Sasaki Kenji San, Mkurugenzi Mtendaji wa Chymia Consulting, Catherine Muraga na Mkurugenzi Mtendaji wa Microsoft ADC, Dk Nkundwe Mwasaga.
Wengine ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama ya Tanzania, Patricia Ithau, Mkurugenzi Mtendaji wa WPP Scangroup PLC, Victor Agolla, Ofisa Mkuu, Ubunifu na Uchumi wa Dijitali wa Serikali ya Kaunti ya Nairobi, na Immaculate Kassait Kamishna wa Data, Ofisi ya Kamishna wa Data Kenya.