Vijana wahamasishwa kushiriki Sensa

Muktasari:

Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM), imezindua kampeni ya kuhamasisha vijana wa maeneo mbalimbali kushiriki Sensa itakaofanyika Agosti 23 mwaka huu.


Dar es Salaam. Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM), imezindua kampeni ya kuhamasisha vijana wa maeneo mbalimbali kushiriki Sensa itakaofanyika Agosti 23, 2022.

Katibu Mkuu wa UVCCM, Kenani Kihongosi amezindua kampeni hiyo Alhamisi, Juni 23, 2022 katika viwanja wa Mwembe Yanga,Temeke. Kabla ya uzinduzi huo vijana wa UVCCM wapatao 3000 wa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, walifanya matembezi ya kutoka Uwanja wa Mkapa hadi Mwembe Yanga.

Hatua ya UVCCM ni mwendelezo wa kuungana mkono jitahada za viongozi wakuu wa Serikali akiwemo Rais wa Samia Suluhu Hassan ambaye katika hotuba mbalimbali amekuwa akisisitiza Watanzania kujiandaa kushirika Sensa kwa maendeleo ya Taifa.

 “Tumeamua kuzindua kampeni ili kuuunga mkono jitihada za Serikali kuhusu Sensa sambamba na kuhamasisha vijana na Watanzania kushiriki mchakato huu. Jambo jingine Sensa ni muhimu kwa Taifa kwa sababu inachochea maendeleo ya nchi.

 “Serikali inapotambua idadi ya wananchi wake ni dhahiri itapeleka fedha au kulingana na idadi hiyo. Wajibu wa UVCCM kuunga jitihda za Serikali za kuwaeleza Watanzania na vijana wenzetu kwa Sensa ni muhimu na inasaidia kusukumu gurudumu la ajenda ya maendeleo,” anasema Kihongosi.

Kihongosi amewasisitiza vijana katika maeneo mbalimbali kujitokeza kwa wingi kushiriki Sensa, sambamba na kuhamasisha wananchi wengine kuhusu umuhimu wa mchakato huo wenye faida mbalimbali.

 “Uzinduzi wa leo umeambatana na wakufunzi wa Serikali na kuna wasanii wametunga nyimbo zenye maudhui ya kuelimisha na kuhamasisha umuhimu wa Sensa.Kampeni hii itakuwa endelevu tukitoka Dar es Salaam tutakwenda katika mikoa yote ya kanda ya ziwa, kaskazini na kusini ili kuwaamsha wananchi kuhusu Sensa,”amesema Kihongozi.




Kampeni hiyo, imehudhuriwa na wenyeviti na makatibu wa UVCCM kutoka katika mikoa mbalimbali nchini ukiwamo wa Lindi na mwenyeji Dar es Salaam.