Vijana wanavyoipa kisogo mahari

Muktasari:
- “Naishi na mwanamke mwaka wa tatu huu hatujafunga ndoa, nilienda kwao kujitambulisha wakaniambia mahari milioni tano, kiukweli nimeachana nao, hiyo hela si naweza kupata gari kabisa. Tulichofanya tumeamua kuzaa, najua watashusha tu, wakigoma basi wamchukue mtoto wao nibaki na mtoto wangu.”
“Naishi na mwanamke mwaka wa tatu huu hatujafunga ndoa, nilienda kwao kujitambulisha wakaniambia mahari milioni tano, kiukweli nimeachana nao, hiyo hela si naweza kupata gari kabisa. Tulichofanya tumeamua kuzaa, najua watashusha tu, wakigoma basi wamchukue mtoto wao nibaki na mtoto wangu.”
Hii ni kauli ya kijana anayeshindwa kurasimisha uhusiano na mwanamke anayeishi naye kutokana na changamoto ya mahari.
Anachopitia kijana huyu ni mfano wa maisha ya vijana wengi wanaokumbana na mzigo mkubwa wa mahari pale wanapotaka kuoa na kuanzisha familia.
Hali hii inawafanya kuishia kuishi bila kufuata taratibu, huku lawama zikitupwa kwa wazazi kuchangia kuweka ugumu katika kuwafanya vijana waingie kwenye ndoa na matokeo yake huishia kutafuta njia za mkato.
Jamii inasemaje?
Akizungumzia hilo, Zahir Matambwe (60) anasema mahari ni utamaduni wa jamii kwa maana binti anayetolewa mahari anawaheshimisha wazazi wake kwa kufuata mila na desturi za Kitanzania.
“Mimi ni Mnyamwezi, ninachofahamu ili binti aolewe ni lazima atolewe mahari ambayo wazazi wake watakuwa wameridhia, inaweza wasiwe baba na mama ila wajomba, mashangazi na baba wadogo wakachukua jukumu hilo. Kwa kifupi ni utaratibu ambao upo na ulikuwepo,” anasema Matambwe.
“Siku hizi naona mambo yanaanza kuwa tofauti, suala hili kama linalegalega halipewi kipaumbele kabisa, yaani imekuwa si ajabu kwa binti kuhamia nyumbani kwa mwanamume bila kutolewa mahari. Ajabu ni kwamba na familia yake inajua kabisa mtoto yupo wapi na wanamtembelea, sasa unajiuliza hivi hawa wanakwenda pale kwa utaratibu upi,” anasema Matambwe.
Hilo linaungwa mkono na Maria Mushi (65), akisema miongoni mwa mambo yanayopotoshwa maana ni mahari na hili linatokana na vijana wengi kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu hili.
“Mtoto wa kike ili uwape heshima wazazi wako pale unapopata mwenza wa maisha ni lazima zifuatwe taratibu zote za kukufanya ukaungane na familia hiyo, miongoni mwa taratibu hizo ni kuposwa na kutolewa mahari, kisha kufunga ndoa kwa kupewa baraka za Mungu kwa ajili ya kuanzisha familia mpya,” anasema Maria.
“Cha ajabu siku hizi mambo yanafanyika kienyeji, watoto wa kike wanajirahisisha na vijana wa kiume wanajilemaza, yaani anakuwa tayari kuishi na mtoto wa watu bila kutoa mahari, hapa ina maana hana ridhaa ya wazazi wa huyo binti.”
Mkazi wa Ilala, Suleima Said anasema wakati mwingine vijana huingia uvivu wa kutoa mahari ili kuoa kwa sababu wengi huanza kuishi kama mume na mke bila kufuata taratibu za kimila wala dini.
“Siku hizi kijana akimaliza chuo anahama nyumbani na kupanga, sasa huko ndipo atakapokuwa akimkaribisha mpenzi wake kwa kuwa yupo huru, na wakati mwingine mpenzi anahamia kabisa, mwisho wa siku wanaishi kama mume na mke,” anasema Said.
Anasema ikishafikia hatua hiyo, mwanamume anaanza kumuona mwanamke wake ni wa kawaida sana, matokeo yake wanaishi bila ndoa kwa kuwa hajamtolea mahari.
Viongozi wa dini
Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Richard Hananja anasema kwenye dini ya Kikristo mahari ni asante ambayo mwanamume anatoa kwa mwanamke anayetaka kumuoa, akimshukuru kwa kupokea ombi lake na kwa shukrani hizo zinaenda pia kwa wazazi.
“Hata kwenye Biblia mahari imeandikwa na hii inatolewa kama asante kwa binti na familia yake kuonyesha unajali na kuthamini kwa kukubali ombi la kukupatia binti yao, haina maana umemnunua. Hii ni hatua ya mwisho ya urafiki baina ya watu wawili wenye lengo la kuanzisha familia, ndipo mahari inapotolewa kama ushahidi kabla ya kuingia kwenye ndoa,” anasema Mchungaji Hananja.
Pia, anasema mahari ina muhimu wake kwa kuwa mwanamke ni kiumbe mwenye thamani na hilo linathibitika kwa kile anachoenda kufanya kwenye ndoa, yeye ndiye anakuwa msingi wa kutengeneza familia.
“Bila mwanamke hakuna familia, yeye ndiye anabeba ujauzito, analea watoto na kujenga familia, si busara kupata kiumbe chenye thamani hii bure na ndiyo maana kuna mahari, ingawa pia haitakiwi iwe ya kumkomoa muoaji. Nasisitiza lengo ni asante, sio kuuza au kununua mtu,” anasema Mchungaji Hananja.
“Changamoto ninayoiona kwa vijana wa sasa hawazungumzi na wazee, hivyo wanafanya mambo vile wanavyoona ni sawa, kumbe wanakosea. Unaenda ukweni unatajiwa mahari Sh5 milioni na wewe unakubali bila neno unailipa yote au inabaki kidogo ukiamini kwamba ndiyo utaonekana uko vizuri kiuchumi.”
Mchungaji anasema kiutaratibu hata kama muoaji ana uwezo wa kulipa mahari iliyotajwa inashauriwa kuomba ipunguzwe kuonyesha unyenyekevu na uhitaji wako wa mwanamke unayetaka kutengeneza naye familia.
“Haya mambo ya watoto wanasoma shule za bweni, wakimaliza wanaenda vyuoni halafu haraka wanakimbilia kuoa yanaleta changamoto kwa namna moja au nyingine. Hawapati yale mafundisho wanayopaswa kuwa nayo vijana na hii ni kwa sababu hawakai na wazee wakawafunza,” anasema Mchungaji Hananja.
Msemaji wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka anasema mahari ni zawadi ya mume kwa mke.
Anasema kwa mujibu wa Kuraan tukufu, falsafa ya kupeana zawadi ni kupendana na Mtume Muhammad amewataka wanaume kuwapa wanawake.
Kuhusu ughali wa mahari, Sheikh Mataka anasema, “ughali wa mahari ni kikwazo kwa vijana kuoa, hasa wale walio mafukara miongoni mwao. Hili la kushindwa kuoa huwasababisha kutokuwa na hiari ila kufuata njia mbaya na chafu ya shetani.
“Na kujikuta tayari wameshatumbukia katika tendo vunda la zinaa aliyo iharamisha Allah.”
Sheikh Mataka anasema hakuna baraka wala kheri, pale mahari itakapokuwa biashara ya kutafutia faida, akisisitiza kuwa ughali wa mahari ni jambo chukivu katika sheria na wepesi katika mahari ni chanzo cha baraka kwa wanandoa na jamii kwa jumla.
Je, mahari haimalizwi?
Hili linafafanuliwa na Maria, akisema wakati mwingine mahari haimaliziwi kwa lengo la kuendeleza ushirikiano baina ya familia hizo, ila haina uhusiano wa moja kwa moja na hali ya uchumi ya mhusika.
“Inawezekana kabisa unacho kiwango chote ulichotajiwa, lakini kiungwana unatakiwa kuonyesha umepungukiwa walau kidogo na yale majadiliano ya kuomba upunguziwe au utamalizia kiasi kilichobakia wakati mwingine yanazidi kuziunganisha familia na kuwa kitu kimoja,” anasema Maria.
Kuhusu familia zinazoweka kiwango kikubwa cha mahari, Mchungaji Hananja anasema hiyo inatokana na namna inayoona inastahili asante ya kiasi hicho, ingawa haitakiwi kuwekwa kiwango ambacho kinaonekana kabisa kumuumiza mhusika.
Suala la kudai kiasi cha mahari kilichobaki ikitokea mke amefariki dunia mchungaji huyo anasema, “hii sio sawa, nikizungumzia upande wa dini ya Kikristo, ninavyofahamu kinachowatenganisha wanandoa ni kifo, sasa kama kifo kimeshatokea hiyo mahari iliyobaki inadaiwa ili apewe nani na kwa sababu gani. Ndoa inapofungwa tayari familia mbili zinakuwa zimeungana, sasa kama mmekuwa wamoja kuzuia maiti au kumnyima mume haki ya kumzika mkewe kwa sababu ya mahari iliyobaki hili halipo kwenye Ukristo.”