Vijana wenye ulemavu wapewa mbinu uhifadhi mazingira, kilimo
Muktasari:
Vijana wenye ulemavu wa viungo na wazazi wa watoto wenye ulemavu wa akili Wilaya ya Nzega mkoani Tabora wamepewa mbinu za kutunza mazingira pamoja na kufanya kilimo cha mviringo ili kujipatia kipato na kuendesha familia zao.
Tabora. Vijana wenye ulemavu wa viungo na wazazi wa watoto wenye ulemavu wa akili Wilaya ya Nzega mkoani Tabora wamepewa mbinu za kutunza mazingira pamoja na kufanya kilimo cha mviringo ili kujipatia kipato na kuendesha familia zao.
Akizungumza wakati wa kuwajengea uwezo Juni 5, 2023 ikiwa ni kuadhimisha siku ya mazingira duniani, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Akili Platform linalojihusisha na afua ya afya ya akili, mazingira na haki za binadamu nchini, Roghat Robert amesema lengo ni kuinua uchumi wa vijana na watu wengine wenye ulemavu kupita kazi za mikono.
Roghat amesema siku hiyo kaya 15 na vijana 10 wamepewa mbegu za karoti, beetroots, papai, pilipili, na mazao mengine huku akiwaomba watanzania kuungana na shirika hilo kuwezesha mbegu za mazao hayo ili kaya na vijana wengi zaidi wasambaziwe na kufanya shuguli za kilimo.
“Kila familia tunalenga kufikia 2025 iwe na uwezo wa kuzalisha kipato yenyewe kupitia shuguli za kilimo,”amesema
Katibu wa chama cha watu wenye ulemavu wa akili Wilaya ya Nzega, Daudi Yassin ameomba kituo cha ushauri na unasihi kianzishwe wilayani humo akidai huduma hiyo haipo na ni muhimu kwa wakazi wa eneo hilo.
Naye Mwenyekiti wa Chawata Wilaya ya Nzega, John Poneka ameomba kituo cha mazoezi ya viungo na semina ya afya ya akili kwa watu wenye ulemavu itolewe zaidi akidai wengi wanashida ya utegemezi kulingana na jinsi walivyo.
Akijibu maombi hayo, Roghat amesema yupo tayari kuungana nao katika hali zote kuhakikisha anaondoa umasikini wa fikra kwa watu wenye ulemavu na mitazamo hasi huku akiahidi kufanyia kazi suala la kituo cha ushauri na unasihi ili huduma itolewe kwa vitendo.