Visima 44 vyagunduliwa kuwa na gesi asilia Tanzania

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Charles Sangweni akizungumza na waandishi wa habari.
Muktasari:
Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania imechimba visima 96 vya utafutaji wa mafuta ambapo 44 vina gesi asilia
Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania, imefanikiwa kuchimba visima vya utafutaji wa mafuta 96 ambapo kati ya hivyo 44 vimegundulika kuwa na gesi asilia.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa PURA, Charles Sangweni jijini Dar es Salaam leo Novemba 19, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na maendeleo ya mamlaka hiyo.
Sangweni amesema kati ya visima hiyo 96 vilivyochimbwa 59 ni vya nchi kavu na 37 vilichimbwa baharini. Kati ya hivyo 44 vilivyogundulika kuwa na gesi asilia vya nchi kavu ni visima 16 na baharini vikiwa 28.
Amesema ugunduzi huo umewezesha kuanza kutumika kwa gesi asilia kama chanzo cha nishati hususan kwa kuzalisha umeme viwandani, majumbani na kwenye magari.
“Uzalishaji wa gesi asilia ulianza mwaka 2004 kwa upande wa maeneo ya SongoSongo na mwaka 2006 kwa upande wa Mnazi Bay, hadi sasa kiasi cha gesi kinachozalishwa kinachangia karibu asilimia 60 ya umeme unaozalishwa hapa nchini,” amesema.
Aidha amesema gesi iliyogunduliwa nchi kavu na kina kirefu cha bahari ni futi za ujazo trilioni 57.54 ambapo kati ya hizo nchi kavu ni trilioni 10.06 na baharini ni trilioni 47.48.
“Uwepo wa gesi hii na hasa iliyogunduliwa katika eneo la bahari kuu, kumesababisha Serikali yetu kuingia kwenye mazungumzo ya utekelezaji wa mradi wa usindikaji wa gesi hiyo kuwa katika hali ya kimiminika, mradi ambao utaliletea taifa manufaa makubwa,” amesema
Hata hivyo amesema utafutaji wa mafuta na gesi unafanyika kupitia mikataba ambayo PURA inaingia na kampuni za kutoka nchi za nje na kuongeza kuwa mikataba hiyo wanaiita ni ya ugawanaji mapato.
“Hii mikataba uwa tunaingiana kampuni kubwa zinazokuja nchini kuwekeza fedha zao na wanachokitafuta kikipatikana tunakaa na kukubaliana namna ya kugawana huku wakirudisha fedha ambazo wamewekeza,” amesema
Amesema kampuni hizo pale zinapokosa kile wanachokitafuta mikataba hiyo imetoa nafasi ya wao kuondoka nchini bila kudai chochote kile ila nchi ubaki na taarifa pamoja na takwimu ambazo zinakusanywa wakati wote wa utafutaji.
Sangweni amesisitiza kuwa hadi sasa maeneo ambayo tayari wameshayafanyia utafiti ni Kilomita za mraba 534,000 ambapo kati ya hizo Km 394,000 zipo nchi kavu na Km 140,000 zipo baharini.