Vituo sita vyatengwa kusaidia waandishi

Muktasari:

Baraza la Habari nchini Kenya (MCK) limeandaa vituo sita kwa vyombo vya habari na waandishi wa habari kwa ajili ya kuwapa mazingira bora na wezeshi wakati wa kuripoti taarifa na matukio yote kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Agosti 9, 2022.

Nairobi. Baraza la Habari nchini Kenya (MCK) limeandaa vituo sita kwa vyombo vya habari na waandishi wa habari kwa ajili ya kuwapa mazingira bora na wezeshi wakati wa kuripoti taarifa na matukio yote kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Agosti 9, 2022.

Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi na Katibu Mkuu wa MCK, David Omwoyo imevitaja vituo hivyo ni Kaunti ya Nakuru, kituo kitakuwa kwenye hoteli ya Kunste,Kaunti ya Uasin Gishu, kituo kitakuwa kwenye hoteli ya Starbucks (Eldoret) huku Kaunti ya Mombasa kituo kitakuwepo kwenye shule ya Serikali ya Kenya.

Vituo vingine vitakuwa kwenye Kaunti ya Kisumu (eneo la Chizoba), Kaunti ya Meru (hoteli ya Elsa) na Kaunti ya Nyeri kituo kitakuwa kwenye hoteli ya White Rhino. MCK imesema kuwa vituo hivyo vitafanya kazi kuanzia Agosti 7 hadi 10 mwaka huu.

“Kuanzia Agosti 7 hadi 10 waandishi wa habari watapatiwa huduma ya kiufundi, vifaa na taarifa zinazohusiana na masuala ya uchaguzi. Pia vituo vitakuwa na intaneti ya haraka na kasi itakayowezesha upashaji wa habari kwa wakati,” imesema taarifa hiyo ya MCK.

Baraza pia limewataka waandishi wa habari wote walioidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) watakaotumia vifaa hivyo kufuata weledi wakati wote wa kuripoti uchaguzi huo.

Baraza hilo ili kuimarisha usalama wa waandishi wa habari litaweka wasimamizi 150 wa kuangalia hali ya uhuru wa vyombo vya habari na waandishi wa habari wakati wote wa shughuli za uchaguzi.

Hii inakuja wiki moja baada ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kupeleka timu ya waangalizi itakayosimamia haki, usawa na uhuru wa vyombo vya habari inayoongozwa na Rais wa awamu ya nne wa Tanzania Jakaya kikwete.