Vodacom Tanzania yapata bosi mpya wa 10

Muktasari:
- Kampuni ya Vodacom imemtangaza Sitholizwe Mdlalose kumrithi Hisham Hendi atakayeachana na kampuni hiyo kuanzia Novemba mosi.
Dar es Salaam. Kampuni ya Vodacom imemtangaza Sitholizwe Mdlalose kumrithi Hisham Hendi atakayeachana na kampuni hiyo kuanzia Novemba mosi.
Mdlalose, raia wa Zimbabwe atakuwa mkurugenzi mtendaji wa 10 wa kampuni hiyo iliyoanza kutoa huduma za mawasiliano nchini miaka 21 iliyopita.
Taarifa ya uteuzi huo imetangazwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Vodacom, Jaji Thomas Mihayo siku 21 tangu alipoujulisha umma kuhusu kuondoka kwa Hendi, Agosti 4.
“Ni kiongozi makini mwenye ubunifu wa kuongoza kampuni yenye hadhi ya kimataifa. Analeta uzoefu mpya alionao katika kukuza biashara kimkakati,” amesema Jaji Mihayo.
Mdlalose, anachukua nafasi hiyo akitoka kuwa mkurugenzi wa fedha wa kampuni ya Vodacom Group alikokuwa akisimamia biashara ya kimataifa. Alijiunga Vodacom Group akitokea Vodafone Group alikodumu kwa zaidi ya miaka sita akishika nafasi kadhaa za uongozi.
Soma zaidi: Bosi Vodacom Tanzania aachia ngazi
Mpaka anakuja Tanzania, mkurugenzi huyo ana uzoefu wa zaidi ya miaka 19 kwenye masuala ya fedha, menejimenti, na ushauri wa uendeshaji wa kampuni. Katika uzoefu huo, miaka 13 ni ameupata kwenye sekta ya mawasiliano kutoka katika nchi zinazoendelea na zilizoendelea.
Mdlalose ni mhitimu wa shahada ya sayansi katika uhasibu (BCompt) ya Chuo Kikuu cha South Africa ambaye ni mhasibu anayetambulika kimataifa akiwa na cheti cha (ACCA). Amefuzu programu ya watendaji waandamizi Afrika inayotolewa na Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Harvard kilichopo nchini Marekani.
Mdlalose anakuwa Mzimbabwe wa kwanza kuiongoza Vodacom Tanzania akiungana na Watanzania wawili walioianzisha ambao ni James Rege na Idris Rashid waliofuatiwa na Waafrika Kusini wanne akianza Bruce Sherwood halafu Jose de Santos akaja Romeo Kumalo na Dietlof Mare.
Baada ya hapo alipita Rene Meza kutoka Paraguay kisha Muingereza Ian Ferrao na Hisham Hendi kutoka Misri.
Mdlalose anatarajia kuanza kutekeleza majukumu yake ya kuiongoza Vodacom kuanzia Novemba mosi, Hendi atakapokuwa anaelekea Hispania kwenda kusimamia majukumu mapya ndani ya kampuni ya Vodafone nchini humo.
Soma zaidi: Bosi wa Vodacom Tanzania afikishwa mahakamani