Wabunge waliotimuliwa Chadema watinga Baraza Kuu

Wabunge waliotimuliwa Chadema watinga Baraza Kuu

Dar es Salaam. Mwezi mmoja tangu wabunge 19 wa Viti Maalum waliokuwa wanachama wa Chadema kufukuzwa licha ya kuapishwa na Spika wa Bunge ili kuitumikia nafasi hiyo, wamekata rufaa kupinga uamuzi wa kuvuliwa uanachama utakaomaanisha kuikosa nafasi hiyo ya uwakilishi bungeni.

Wabunge hao wakiongozwa na aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee walifukuzwa uanachama Novemba 27 na Kamati Kuu ya chama hicho baada ya kwenda kuapishwa kuchukua nafasi 19 za ubunge wa viti maalum ambazo zilizosusiwa na chama hicho kinachopinga matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Pamoja na kufukuzwa huko, wabunge hao walikuwa na haki ya kukata rufaa ndani ya mwezi mmoja kwa mujibu wa katiba ya chama hicho na jana ndiyo ulikuwa mwisho wa kupokea rufaa zao.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu, mkurugenzi wa mambo ya nje, itikadi na uhusiano wa Chadema, John Mrema alisema mpaka jana asubuhi wabunge 13 walikuwa wamepeleka barua za kukata rufaa katika ofisi za makao makuu ya chama hicho zilizopo Mtaa wa Ufipa Kinondoni jijini hapa.

“Mpaka leo asubuhi walioleta rufaa ni 13. Tunasubiri hadi saa 10 jioni kujua wangapi wataleta kwani bado muda wanao,” alijibu Mrema kwa ujumbe mfupi wa maneno.

Hata hivyo, alipotafutwa kuanzia saa 10 jioni ili kujua kama warufani hao wameongezeka ama la, hakupatikana tena kwenye simu yake.

Juhudi za kumpata katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika nazo hazikufanikiwa kwani simu yake iliita bila kupokelewa.

Mbali na Mdee, wabunge wengine waliofukuzwa uanachama ni Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnesta Lambert, Nusrati Hanje na Jesca Kishoa.

Wengine ni Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Nagenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.

Katiba ya Chadema

Ibara ya 5.4.3 ya katiba ya Chadema inaelezea mchakato wa kukoma uanachama na nafasi ya kukata rufaa kwamba hutokana na “kuachishwa ama kufukuzwa na tawi lake ama ngazi nyingine ya chama kwa mujibu wa katiba, kwa kukosa sifa za kuendelea kuwa mwanachama ama kuwa na mwenendo usioendana na itikadi, falsafa, madhumuni, kanuni, maadili na sera za chama.

“Mwanachama atakuwa na haki ya kukata rufaa kwa ngazi za juu kama hakuridhika na adhabu hiyo.”

Kwa kuwa wabunge hao walifutiwa uanachama wao na Kamati Kuu, wanatakiwa kukata rufaa Baraza Kuu ambalo kwa mujibu wa ibara ya 7.7.3 (e) ya katiba ya Chadema lina jukumu la “kusikiliza na kutoa uamuzi juu ya rufaa za uchaguzi na kinidhamu kutoka ngazi za chini.”

Endapo Baraza litashikilia msimamo wa Kamati Kuu, akina Mdee bado watakuwa na nafasi ya kukata rufaa katika Mkutano Mkuu ambao kwa mujibu wa katiba ya chama hicho ibara ya 7.7.10 (f), kazi yake ni pamoja na “kuzingatia na kutoa uamuzi juu ya rufaa na masuala ya kinidhamu yanayowasilishwa na Baraza Kuu.”

Endapo Mkutano Mkuu nao utashikilia uamuzi huo, wabunge hao wanaweza kwenda mahakamani wakitaka.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Desemba mosi, wabunge hao walisisitiza kuendelea kuwa wanachama wa Chadema wakijiita ‘wanachama wa hiyari.’

“Sisi tutakuwa wanachama wa hiyari, tutafanya taratibu za ndani ya chama kwa mujibu wa katiba. Mamlaka ya rufaa ni kikao cha juu kwa maana ya Baraza Kuu kilichofanya uamuzi.

“Tunakipenda Chadema, tunakiheshimu Chadema, hatutaondoka Chadema, tutabaki wanachama wa hiyari mpaka tutakapokwenda kujadili mambo yetu ya ndani na kuyamaliza,” alisema Mdee.

Mdee hakupatikana jana kulizungumzia suala la wao kukata rufaa ndani ya chama hicho. Akitangaza kuwafukuza uanachama wabunge hao, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema licha ya chama hicho kukataa kupeleka majina ya makada wanaostahili uteuzi wa viti maalum kwenda Tume ya Taifa ya Uchaguzi, hatua ya wabunge hao kwenda kuapishwa imeenda kinyume na Katiba ya Tanzania.

Alivitaja vifungu vilivyokiukwa ni ibara ya 78 (3) inayosema majina ya waliopendekezwa na tume yatatangazwa kama matokeo ya uchaguzi baada ya tume ya uchaguzi kuridhika kwamba sheria imezingatiwa.

Ibara nyingine ni ya 67 (1b) inayoweka masharti na sifa ya mtu kuteuliwa kuwa lazima apendekezwe na chama cha siasa.