Wabunge watia mkono sakata tozo
Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde,
Muktasari:
- Wakati wadau mbalimbali wakiwanyooshea kidole wabunge kwa kupitisha sheria inayoruhusu tozo za miamala ya kielektroniki, baadhi ya wabunge wametetea tozo hizo, huku wakisema suala la kiwango cha tozo linazungumzika.
Dar es Salaam. Wakati wadau mbalimbali wakiwanyooshea kidole wabunge kwa kupitisha sheria inayoruhusu tozo za miamala ya kielektroniki, baadhi ya wabunge wametetea tozo hizo, huku wakisema suala la kiwango cha tozo linazungumzika.
Hata hivyo, wengine walisema alichokizungumza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ni kwa niaba ya Bunge, hivyo maoni yake yachukuliwe kama msimamo wao.
Juzi Dk Mwigulu alisema: “Tulikuwa kimya tukisikiliza maoni ya wananchi na hii si mara ya kwanza kupokea maoni ya wananchi… moja kubwa ambalo tumeona ni kutozwa mara mbili, Serikali imesikia hiyo hoja na ni hoja ya msingi kweli kweli.”
Takribani wiki mbili, maeneo mbalimbali, ikiwemo mitandaoni, kumetawala mjadala kuhusu tozo, hata hivyo, Septemba 2, Dk Mwigulu alijitokeza hadharani kufafanua kuhusu tozo hizo na kukiri maoni yaliyotolewa na wadau ni mazuri na watayafanyia kazi ndani ya kipindi mfupi kijacho.
Katika mjadala huo, Bunge ambalo lina wabunge wengi wa CCM, limekuwa likilaumiwa kwa kupitisha sheria ya kodi ambayo imeruhusu tozo hizo, jambo ambalo linatetewa na baadhi ya wabunge, wakisema wananchi lazima walipe kodi kwa maendeleo ya nchi.
Miongoni mwa waliozungumza jana na gazeti hili ni Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, aliyesema kazi ya wabunge ni kupitisha sheria ya kodi na siyo kupitisha kiwango cha kodi au tozo, huku akiwataka wananchi kutambua hilo, lakini pia kuwa tayari kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
“Wabunge kazi yetu ni kupitisha sheria ya kuwatoza wananchi kodi, tukiwamo na sisi kama sehemu ya wananchi. Na hii nchi ni yetu, kumbe hela tutapata wapi! Lakini kiwango cha tozo, siyo kazi ya mbunge,” alisema Lusinde.
Lusinde aliungwa mkono na Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu aliyesema nchi hii itajengwa na Watanzania wenyewe na hakuna mahali ambako Serikali inategemea kupata fedha zaidi, ila kwa Watanzania wenyewe kulipa kodi.
“Kama imetokea changamoto labda tozo ni kubwa au nini, ndiyo Serikali inaangalia namna ya kurekebisha, lakini kwamba tusilipe kodi haitawezekana. Tunahitaji maji yafike kila mahali, tunahitaji elimu, Serikali inapeleka umeme vijijini,” alisema.
Aliongeza kutokana na maendeleo ya teknolojia, biashara imehamia mtandaoni na kwamba Serikali imejenga mkongo wa Taifa wa mawasiliano ambao unahitaji matengenezo ili mawasiliano yafike sehemu zote za nchi.
“…Lakini kama tozo ni kubwa hapo ni kufanya adjustment (marekebisho) kutokana na hali za wananchi zilivyo, lakini kwamba tusilipe kodi, tutaishi vipi?” alisema Msambatavangu wakati alipozungumza na Mwananchi.
Walichokisema wabunge hao kinafanana na kauli ya Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka aliyesema hali ya maisha duniani kote ni ngumu kutokana na mfumuko wa bei uliosababishwa na vita kati ya Russia na Ukraine pamoja na mlipuko wa Uviko-19 na kwamba mfumuko huo hauna uhusiano wowote na tozo.
“Tozo ukiziangalia, hazina impact (athari) kubwa kiasi hicho wanachokizungumza; tozo zenyewe zina manufaa makubwa, sasa hivi mambo makubwa yamefanyika,” alisema mbunge huyo kupitia CCM.
Alibainisha kinachoendelea ni upotoshaji na kwamba watu wanajaribu kuangalia hali ya ugumu wa maisha na kuihusianisha na tozo badala ya kuwaeleza wananchi ukweli kuhusu chanzo kuwa ni mfumuko wa bei.
“Kwangu mimi, huwezi kuniambia tozo ndiyo imeleta hizo shida, pamoja na kwamba ni kweli kwa kiasi fulani, na hili linazungumzika kwa sababu hata huko nyuma zilishapunguzwa sana,” alisema Kuchauka.
Alisisitiza kwamba ni kweli wananchi wanapitia maisha magumu katika kipindi hiki, lakini ugumu huo umeletwa na bei ya mafuta kwenye soko la dunia. Alisema Rais Samia anatoa ruzuku kwenye mafuta lakini bado hayajashuka, na kwa nchi ambazo hazina ruzuku hiyo, alidai bei iko juu zaidi.
Mbunge wa Chemba, Mohamed Monni alisema kuwa anaaamini tozo hizo zimewezesha ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Hata hivyo, alisema jambo hilo limefafanuliwa vizuri na mawaziri.
“Ungeniuliza kabla ya mawaziri kuzungumza ningekuwa na cha kuzungumza. Lakini Waziri wa Fedha (Dk Mwigulu) na mawaziri wengine wamejieleza vizuri kuhusiana na umuhimu wa tozo. Waziri ni mbunge, alipoleta bungeni tulijadili kwa kina kabla ya kupitisha,” alisema.
Alisema Serikali haina duka la kuzalisha fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo, inategemea kodi na tozo ili kuendesha miradi mbalimbali.
“Ingekuwa wanakusanya fedha halafu hatuoni kinachofanyika hapo sawa lakini miradi inayotekelezwa inaonekana. Chukueni muda (waandishi wa habari) kuwaelimisha watu kuhusu umuhimu na faida ya tozo,”alisema.
Alitoa mfano bajeti ya jimbo lake imeongezeka kutoka Sh700 milioni hadi Sh1.5 bilioni kwa sababu ya tozo na isingekuwa hizo tozo wasingeweza kujenga kituo cha afya na miradi mingine.
Alisema kuwa Watanzania wengi hawana utamaduni wa kulipa kodi na hivyo ni watanazania wachache ndio wanalipa kodi lakini wote wanakwenda kwenye zahanati.
Kwa upande wake, Mbunge wa Tumbe, Amour Khamis Mbarouk alisema asingependa kuzungumzia suala hilo kwa sababu limehitimishwa na Waziri wa Fedha juzi wakati
“Kuhusu hili, Waziri alishatamka, kwa sababu akishakuwa waziri, yeye pia ni mbunge, kwa hiyo yeye alichokisema, kalisemea Bunge, kaisemea Serikali, kaisemea nchi. Kwa hiyo sina maneno mazuri zaidi ya yale aliyoyasema Waziri (Mwigulu),” alisema.
Akiwa na mtazamo kama huo, mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate alisema hawezi kuzungumza jambo hilo kwa sababu lilishasemwa na Waziri mwenye dhamana hivyo kwake inakuwa vigumu.
“Siwezi kulisemea jambo hilo kwa sasa, Waziri mwenye dhamana (Dk Mwigulu Nchemba) ameshalisema kwa hiyo kuongea Mimi kama sheria nzuri au mbaya ni kuwachanganya wananchi wetu,” alisema Bilakwate.
Akizungumza hilo, mmoja wa wabunge wa mkoa wa Kilimanjaro ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema wao kama wabunge wana sehemu ya kusemea na kuishauri serikali namna ya kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi.
“Sisi kama wabunge tuna kinga ya bunge,tuna sehemu ya kuyasemea haya na kuishauri serikali ili kuona ni namna gani ya kupunguza ukali wa maisha na kuleta ahueni kwa wananchi,” alisema mbunge huyo.
Imeandikwa na Peter Elias (Dar), Sharon Sauwa (Dodoma) na Janeth Joseph (Moshi).