Wabuni mashine inayotoa tiba nne kwa watoto njiti

Muktasari:

  • Imebuniwa na wataalamu wa ndani wa fani ya uhandisi wa vifaa tiba ‘Biomedical Engeneering’, inatoa joto lenye uwiano sawia na lile la tumboni mwa mama, ina uwezo wa kutibu ugonjwa wa manjano, kuonyesha joto na uzito wa mtoto.

Dar es Salaam. Wataalamu sita wa fani ya uhandisi wa vifaa tiba ‘Biomedical Engineering’ nchini wameungana na kubuni mashine ya kuhifadhi watoto waliozaliwa kabla ya wakati ‘Phototherapy Machine’ yenye uwezo wa kutoa tiba nne tofauti kwa mtoto hao.

 Mashine hiyo yenye uwezo wa kutoa joto kama la tumboni mwa mama, kutibu ugonjwa wa manjano, kuonyesha joto na uzito wa mtoto, imebuniwa na wahandisi hao kupitia kampuni mpya ya Tiba Labs wakishirikiana na madaktari bingwa wa watoto wachanga na madaktari bingwa wa wanawake na uzazi.

Wameonyesha mashine hiyo jana Jumapili Aprili 7, 2024 katika mkutano wa kimataifa 2024 WomenLift Health Global unaoangazia masuala ya uongozi kwa wanawake duniani kisekta, Mkurugenzi wa Doris Mollel Foundation, Doris Mollel amesema lengo la ubunifu huo ni kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati maeneo ya pembezoni.

Amesema uwepo mashine hiyo itapunguza gharama na kusaidia kuokoa maisha ya watoto wengi nchini Tanzania.

“Kifaa hiki kimewekwa vitu vinne ndani yake, mojawapo mtoto aweze kupona ugonjwa wa manjano, pia kitamsaidia kupata joto kama la mama, kwani kimewekewa kifaa maalumu kinachozalisha joto. Pia kinaweza kuonyesha uzito wake na mhudumu atajua joto la mtoto likoje,” amesema.

Doris amesema ukilinganisha na vifaa tiba vingine vilivyopo sokoni, mpaka kukamilika kwake mashine hiyo imegharimu Sh1.5 milioni, huku zile zinazopatikana madukani zikiuzwa kwa Sh3.5 milioni mpaka Sh4.5 milioni kutegemea na chapa yake na nchi ilikotengenezwa.

“Mashine hii imewekewa nyenzo zote kupunguza gharama ya matumizi ya ununuzi wa vifaa tiba,” amesema.

Amesema ubunifu huo uliofanywa na Watanzania ukifanikiwa kupitia michakato yote ya ukaguzi na kuonyesha inafaa kwa matumizi, wataiingiza sokoni, kwani lengo kubwa ni kuipeleka katika vituo vya afya vya msingi, ikiwemo zahanati na vituo vya afya.

Doris amesema wamelenga maeneo hayo kwa kuwa hakuna wataalamu wenye stadi za juu na mshine hiyo, ni rahisi kutumia ukilinganisha na mashine nyingine.

“Tunaendelea kuwapongeza wabunifu wetu ambao wameendelea kubuni vifaa rahisi kwa ajili ya kuhudumia Watanzania, pia tunaishkuru Wizara ya Afya kupitia wao tumeweza kuandaa kifaa hiki.

“Pia tunashirikiana katika hatua zinazofuata za kufanya majaribio kwa watoto wachanga na tutaona ni namna gani pia tunavyoweza kuhakikisha zinaingia sokoni na zinatumika na Watanzania kuboresha huduma,” amesema.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel, Doris Mollel akionyesha  mashine  iliyobuniwa na wahandisi wa vifaa tiba alivyoitambulisha kwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Phillip Mpango

Kwa mujibu wa Doris, mashine hiyo inatarajiwa kuchunguzwa na Mamlaka ya Dawa Vifaatiba Tanzania (TMDA) kabla ya kuruhusiwa kutumika.

Akizungumzia tatizo la watoto wanaopata manjano nchini, Doris amesema ni kubwa hasa kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.

“Watoto njiti wengi wanapata manjano, ukiingia katika wodi za watoto wachanga lazima ukutane na mashine ya phototherapy imewaka. Hii inamaanisha tatizo ni kubwa na kwa bahati mbaya watoto hawa wasipopatiwa matibabu kwa wakati wana uwezekano wa kupata mtindio wa ubongo,” amesema.

Akizungumzia mkutano huo, Doris ambaye ni mraghabishi wa huduma za watoto wanaozaliwa kabla ya wakati nchini, amesema bado Tanzania hatuna viongozi wa kutosha kwenye sekta ya afya wanaoweza kuleta matokeo chanya.

Amependekeza kuwa bado nchi inahitaji wanawake wanolewe kuweza kushika nafasi za uongozi katika sekta ya afya.


“Natamani kuona waganga wafawidhi wengi wakiwa ni wanawake, kwenye hospitali zetu kubwa itatupeleka kwenye mafanikio makubwa, wanawake kushika nafasi  kubwa wanatakiwa pia waandaliwe kwa kupata mafunzo waweze kushika nafasi hizo,” amesema.

Mjumbe wa mkutano huo, Verda Msangi amesema wapo tayari kujifunza kutoka kwa wanawake wengine ambao ni viongozi, kwa kuwa bado wanawake wanaweza kuingia kwenye nafasi za uongozi wa juu katika sekta ya afya.

“Tupo hapa pia kujifunza na kuona jinsi gani tutashirikiana, ili kuhakikisha afya ya mwanamke na afya za Watanzania zinaimarika kupitia mashirikiano hayo na mahusiano,” amesema Msangi.

Mkutano huo unaofanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Mwalimu Nyerere JNICC ukishirikisha mataifa zaidi ya 40, unaotarajiwa kumalizika leo umewakutanisha zaidi ya wajumbe 1000 duniani wakiangazia hatua za pamoja kuhusu uongozi wa mabadiliko, ushirikiano kama njia ya usawa wa kijinsia na hatua katika kuendeleza uongozi wa wanawake katika afya ya kimataifa.