Wabunifu waitwa NIT kuongeza ujuzi

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Dk Ally Possi ( wa kwanza kushoto) akikagua moja ya kifaa cha ndege kilichopo katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT)
Muktasari:
Wabunifu nchini wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupata utaalamu katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa lengo la kukuza ubunifu wao ili uendane na soko la kimataifa.
Dar es Salaam. Wabunifu nchini wametakiwa kujitokeza kwa wingi kupata utaalamu katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa lengo la kukuza ubunifu wao ili uendane na soko la kimataifa.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Dk Ally Possi wakati alipofanya ziara katika chuo cha NIT kuona shughuli mbalimbali zinazofanyika chuoni hapo.
Amesema NIT ni sehemu muhimu kwa wabunifu hasa katika sekta ya usafiri kukuza ubunifu wao hatua itakayochangia kutangaza bidhaa au huduma wanazozalisha na kutengeneza katika masoko ya nje.
“Nitoa rai kwa chuo cha NIT, wawatafute wabunifu wote waliopo nchini ili wawawezeshe kupata fungu, watu hawa waweze kuendeleza taaluma na bunifu zao na hatimaye kuja kuendesha miradi mbalimbali iliyopo nchini,” amesema.
Possi amewataka NIT, kuhakiksha kila mwananchi anafahamu huduma wanayoitoa chuoni hapa, kwakuwa amejionea vifaa na vyombo vya kisasa za ufundishaji na ukaguaji magari.
Amesema kwa upande wa Serikali wataangalia utaratibu mzuri ambao utafaa hasa wa magari ya abiria kufanyiwa ukaguzi vizuri kwa lengo la kupunguza ajali za barabarani.
Naye Mkuu wa Chuo cha NIT, Profesa Zacharia Mganilwa amesema katika kupanua wigo wa mafunzo, chuo kimepata eneo la hekta 25 mkoa wa Lindi ambapo wanatarajia kujenga kampasi kwaajili ya kutoa mafunzo ya wajenzi na wasanifu wa meli pamoja na mafundi wa miundombinu ya bandari.
“Kwa upande wa wataalamu wa reli mafunzo yameanzia hapa Dar es Salaam ambapo kwenye upande wa menejimenti ya mashirika ya reli kozi hiyo imeshaanza kutolewa kwa ngazi ya Diploma, lakini tunatoa shahada ya kwanza ya wabobezi wa kuendesha haya mashirika ya reli,” amesema