Wabunifu watakiwa kulinda kazi zao za sanaa
Washiriki wa mafunzo maalumu kwa wabunifu vijana 50 wa sanaa za aina mbalimbali yaliyoandaliwa na Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF) kwa kushirikiana na NEXLaw Advocates pamoja na Ruge Mutahaba Foundation mafunzo yanafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 18 hadi 19, 2026.
Muktasari:
- Wabunifu na wasanii vijana nchini wametakiwa kutambua thamani ya kazi zao za ubunifu kwa kuzilinda kisheria, kuzisimamia kibiashara na kuzitumia kama nyenzo ya kujenga uchumi wao na wa Taifa.
Dar es Salaam. Wabunifu na wasanii vijana nchini wametakiwa kutambua thamani ya kazi zao za ubunifu kwa kuzilinda kisheria, kuzisimamia kibiashara na kuzitumia kama nyenzo ya kujenga uchumi wao na wa Taifa.
Wito huo umetolewa kupitia mafunzo maalumu ya siku mbili kwa wabunifu wa sanaa aina mbalimbali vijana 50 yaliyoandaliwa na Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF) kwa kushirikiana na NEXLaw Advocates pamoja na Ruge Mutahaba Foundation mafunzo yanafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 18 hadi 19, 2026.
Mafunzo hayo yaliyobeba kaulimbiu isemayo: “Your Art, Your Power” yamelenga kuwawezesha wabunifu kwa kuwapatia maarifa ya kisheria, kuwaunganisha na taasisi muhimu pamoja na kuwajengea mitandao ya kitaaluma itakayowawezesha kukuza na kunufaika na kazi zao katika uchumi unaokua wa sekta ya ubunifu nchini.
Pamoja na ukuaji wa sekta ya ubunifu, waandaaji wa mafunzo hayo wanasema wasanii na wabunifu wengi bado wanakabiliwa na changamoto za kulinda, kuuza na kukuza kazi zao kutokana na uelewa mdogo wa haki miliki, mikataba isiyo imara na ukosefu wa msaada wa kisheria.
Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo, Mwanzilishi Mwenza na Mkuu wa Idara ya Haki Miliki katika NEXLaw Advocates, Profesa Saudin Mwakaje amesema wasanii wa Tanzania wanaendelea kuzalisha kazi zenye thamani kubwa ya kiuchumi, hivyo ni muhimu kuwapa zana, maarifa na mitandao itakayowawezesha kumiliki kikamilifu na kunufaika na kazi wanazozalisha.
“Tunahakikisha kila mbunifu kijana anayeshiriki mafunzo haya anatoka akiwa anatambua kuwa kazi yake ya sanaa ndiyo nguvu yake, mali yake na msingi wa maendeleo yake ya kiuchumi,” amesema.
Mtendaji Mkuu wa Ruge Mutahaba Foundation, Elias Tryphone amesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kujenga uchumi wa ubunifu ulio imara, unaolindwa kisheria, unaojiendesha kibiashara na unaoungwa mkono na taasisi mbalimbali.
Msaidizi wa Kitengo cha Ubunifu kutoka Taasisi ya Jakaya Kikwete, Ruth-Sulla King 'ori amesema wamegundua baadhi ya wabunifu kutokuwa na uelewa wa thamani ya kazi zao za ubunifu wanazozifanya, hivyo semina hiyo itawasaidia kuwa kuwakutanisha na taasisi za Serikali zinazosimamia sanaa na ubunifu hapa nchini.
Katika semina hiyo, Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) na Chama cha Hakimiliki Tanzania (Cosota) pia wanatoa mafunzo kwa washiriki hao.