Wadaiwa sugu wa ardhi Ilemela kufikishwa mahakamani

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (Katikati) akimkabidhi mkazi wa Kigoto, John Urio ankara ya kiwanja chake kwa ajili ya kukilipia ili akabidhiwe hati yake. Picha na Mgongo Kaitira.

Muktasari:

Halmashauri ya manispaa ya Ilemela imesema itawafikisha mahakamani wadaiwa sugu 451 walioshindwa  kulipa kodi ya pango ya ardhi.

Mwanza. Halmashauri ya manispaa ya Ilemela imesema itawafikisha mahakamani wadaiwa sugu 451 walioshindwa  kulipa kodi ya pango ya ardhi.

Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo, John Wanga, mkuu wa idara ya ardhi wa manispaa hiyo, Shukrani Kyando amesema wadaiwa hao watafikishwa mahakamani Machi 12, 2021.

“Kuna watu wamemilikishwa ardhi kwa muda mrefu lakini hawalipii kodi matokeo yake halmashauri inapoteza mapato inayostahili kuyakusanya kutoka kwao, tumeshawapatia barua za wito wa kuhitajika mahakamani,” amesema Kyando.

Akizungumzia suala hilo Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewataka wananchi nchini kulipa kodi  ili kuepuka usumbufu ikiwemo kufutiwa hati ya umiliki wake.

“Ni ajabu sana kukuta mtu umeshapewa miliki ya kiwanja chako halafu unashindwa kulipia sasa hivi hatucheki na uzembe wa aina hiyo tukiona umeshindwa kulipia tunakufutia umiliki,” amesema Lukuvi.

Pia.  Lukuvi  Lukuvi amegawa ankara 500 za madeni ya kodi ya ardhi kwa wakazi wa mtaa wa Kigoto kata ya Kirumba mkoani Mwanza ili wakamilishe zoezi la ulipaji kwa ajili ya kumilikishwa jumla maeneo yao.