Wadakwa wakidaiwa kutengeneza pombe 'feki'

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama akionyesha moja ya bidhaa inayotumika kutengeneza pombe kali 'feki'.  Picha na Lilian Lucas

Muktasari:

  • Katika tukio mojawapo, Polisi wamebaini uwepo wa kiwanda kinachodaiwa kuwa bubu kilichopo Mtaa wa Tushikamane, Kata ya Lukobe, Manispaa ya Morogoro kinachotengeneza pombe zisizo halali.

Morogoro. Watu saba wanashikiliwa na Polisi Mkoa wa Morogoro kwa tuhuma tofauti, zikiwemo kumiliki kiwanda bubu cha kutengeneza pombe kali 'feki' na kuzisambaza mtaani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Alex Mkama ametoa taarifa hiyo leo Desemba 29, 2023 alipozungumza na waandishi wa habari na kusema watu hao wamekamatwa katika oparesheni na misako iliyofanywa na jeshi hilo wilayani Morogoro katika kipindi cha Desemba.

Katika tukio la kwanza, Polisi wamebaini uwepo wa kiwanda kinachodaiwa kuwa bubu kilichopo Mtaa wa Tushikamane, Kata ya Lukobe, Manispaa ya Morogoro na polisi wanamshikilia Ramadhani Mdoe (30), fundi na mkazi wa Msamvu na wenzake watatu.

Vifaa vilivyokamatwa vinavyodaiwa kutumuka kutengeneza kutengeneza pombe kali 'feki' mkoani Morogoro. Picha na Lilian Lucas

Kamanda Mkama ametaja bidhaa feki ya pombe kali zilizozotengenezwa na kiwanda hicho ni chupa za Smart Gin 2,544, Konyagi chupa 65, madumu ya lita 20 yaliyojazwa spiriti 4, pipa tupu moja la spiriti, pamoja na dumu sita za lita 20 zenye mchanganyiko wa spirt na maji.

Vitu vingine vilivyokamatwa katika kiwanda bubu ni jaba tatu kwa ajili ya kuchanganya na kuchuja pombe, gundi chupa tano, PM kwa ajili ya Fleva, stika 2,037 za TRA, Lebo 6,226, Smart Gin pamoja na lebo 10,886 za konyagi kubwa na ndogo.

Amesema watuhumiwa wote wanashikiliwa katika kituo kikuu cha polisi Morogoro kwa mahojiano zaidi.

Katika tukio lingine, Richard Paul (39) mkazi wa Kihonda na wenzake wawili wanashikiliwa kwa tuhuma za kufanya shughuli za uganga wa kienyeji bila kibali na kupiga ramli chonganishi, jambo linalochangia kutokea migogoro katika jamii.

Kamanda Mkama amesema watuhumiwa wote wanahojiwa na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.