Wadau wabainisha mambo yatakayochochea utamaduni wa kujisomea vitabu nchini

Muktasari:
- Wadau mbalimbali wametoa mapendekezo yatakayowezesha kuongeza utamaduni wa watu kujisomea vitabu nchini Tanzania ili kuongeza maarifa.
Dar es Salaam. Wadau mbalimbali wametoa mapendekezo yatakayowezesha kuongeza utamaduni wa watu kujisomea vitabu nchini Tanzania ili kuongeza maarifa.
Wadau wamebainisha hayo leo Alhamisi Oktoba 27, 2022 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa maktaba ya Uongozi iliyoenda sambamba na uzinduzi wa kitabu cha Hayati Benjamin Mkapa cha "Maisha Yangu, Kusudi Langu" kilichotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili.
Mjadala ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Ltd (MCL), Bakari Machumu, umewakutanisha wadau kutoka kada mbalimbali ili kutafuta suluhisho la kudumu.
Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kuna haja ya kuondoa kodi kwenye vifaa vyote vinavyohusisha vitu vya kusoma kama vile magazeti, karatasi za kuchapia magazeti au vitabu pamoja na wino.
"Nadhani masuala yote yanayohusu vitu vya kusoma, tuondoe masuala ya kodi ili vitabu viwepo. Vitabu vikiwepo watu watasoma tu," amesema Zitto.
Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo amesema umefika wakati wa kufufua maktaba za jamii ili mwanafunzi aende kujisomea.
"Kinachotakiwa ni kujenga jamii yenye kupenda mawazo mbadala, turuhusu majadiliano kuanzia shuleni na vyuoni. Majadiliano haya yatamlazimisha mtu kusoma tu. Viongozi wetu watengeneze mazingira mazuri ya kujadiliana," amesema Profesa Kitila.
Kwa upande wake, Mkuki Bgoya kutoka kampuni ya uchapaji vitabu ya Mkuki na Nyota, amesema ni muhimu kuhakikisha maktaba za wilaya zinakuwa na vitabu ili watu waweze kwenda kujisomea.
"Tukiboresha maktaba zetu na tukahakikisha zina vitabu, kila mmoja atakwenda kusoma," amesema Bgoya wakati akichangia mjadala huo.
Mhadhiri mstaafu, Profesa Saida Yahya Othman amesema wazazi wawajengee watoto wao utamaduni wa kusoma vitabu badala ya kuwanunulia simu.
"Tufikirie zaidi watoto ambao wanatoka familia za hali ya chini, tufanye vitabu kuwa ndiyo burudani yao," amesema Profesa Saida.