Wadau watoa ya moyoni Serikali kuruhusu “Michomoko”

New Content Item (6)
New Content Item (6)

Muktasari:

Baada ya kuruhusu magari madogo maarufu kama “Michomoko” kusafirisha abiria, wadau wa usafirishaji wamezitaka taasisi na mamlaka husika kusimamia utii na utekelezaji wa sheria za usalama barabarani kudhibiti mwendo kasi na kujaza abiria kupita kiasi kwenye magari hayo.

Mwanza/Bariadi. Baada ya kuruhusu magari madogo maarufu kama “Michomoko” kusafirisha abiria, wadau wa usafirishaji wamezitaka taasisi na mamlaka husika kusimamia utii na utekelezaji wa sheria za usalama barabarani kudhibiti mwendo kasi na kujaza abiria kupita kiasi kwenye magari hayo.

Uamuzi wa kuruhusu “Michomoko” umetangazwa juzi Jumamosi Machi 26 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa ziara yake mkoani Simiyu; takribani miezi tisa tangu yazuiwe na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, David Kafulila.

Kafulila alifikia uamuzi huo Julai 13, 2022 baada ya magari hayo kuhusika katika matukio zaidi ya matano ya ajali za barabarani na kusababisha vifo na majeruhi kadhaa huku magari aina ya Probox yaliyohusika katika ajali hizo kubainika kupakia abiria zaidi ya 10 ikiwa ni mara mbili zaidi ya idadi ya abiria watano inayoweza kubeba.

Madereva wa magari hayo ambayo yalidaiwa kuendeshwa kwa mwendo kasi pia walikiuka masharti leseni ya usajili kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (Latra) kwa kuyageuza kuwa daladala badala ya magari ya kukodi huku baadhi yao wakidaiwa kutozingatia sheria na kanuni za usalama barabarani.

Wakizungumzia uamuzi wa Serikali wa kuruhusu magari hayo kuanza tena kutoa huduma, baadhi ya wadau wa usafirishaji wametaja eneo la utoaji wa leseni kuwa miongoni mwa maeneo yenye udhaifu katika usimamizi unaosababisha wasio na sifa kupata leseni ikiwemo ya kuendesha magari ya abiria.

Ibrahim Maige, mmoja wa madereva wa michomoko mjini Bariadi amesema baadhi ya wanaoendesha magari hayo licha ya kuwa na leseni, hawana sifa za udereva kwa sababu hawajahudhuria mafunzo.

"Utoaji wa leseni una mapungufu yanayotakiwa kurekebishwa. Mfano ni kumwona mtu anajifunza kuendesha chombo cha moto mltaani lakini baada ya muda mfupi anaomba na kupata leseni bila kuwa na uthibitisho wa ujuzi kutoka chuo cha udereva kinachotambulika kwa mujibu wa sheria,” anasema Ibrahim

Mfanyabiashara ndogondogo jijini Mwanza, John Masatu ameunga mkono hoja ya kuiomba Serikali kupitia Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama barabarani na Latra kusimamia utii, usimamizi na utekelezaji wa sheria bila kama njia ya kudhibiti siyo tu uvunjaji wa sheria, bali pia kuokoa maisha yanayopotea kwenye matukio ya ajali zinazoweza kuzuilika.

“Ajali za barabarani zinazozuilika ikiwemo zinazotokana na ukaidi wa sheria kwa kuendesha mwendo kasi, kujaza abiria kupita kiasi na kupuuza alama za barabarani zinaweza kudhibitiwa na Jeshi la Polisi kwa kusimamia utii na utekelezaji wa sheria kwa kila mtumiaji wa barabara,” anasema Masatu

Katibu wa taasisi ya mabalozi wa Usalama Barabarani Mkoa wa Geita, Mohamed Mhando naye amesisitiza umuhimu wa mamlaka husika kusimamia kikamilifu utekelezaji na utii wa sheria za usalama barabarani kama njia ya kudhibiti ajali za michomoko na zingine zote zinazotokana na ukaidi na uzembe wa madereva.

Agizo la Waziri Mkuu

Katika agizo lililotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuruhusu michomoko kuanza kusafirisha tena abiria, Serikali imewaagiza viongozi na mamlaka zote zinazohusika kusimamia utendaji wa magari hayo kwa kuwapa wamiliki na madereva miongozo ya kisheria na elimu ya usafirishaji salama.

“Mkuu wa Mkoa, Ofisi yako ilisitisha matumizi ya magari haya maarufu kama mchomoko….sasa tumefungua milango. Rais Samia Suluhu Hassan alikwishaelekeza hawa wajasiamali wadogo wawezeshwe,” alisema taarifa kwa umma iliyotolewa juzi na Ofisi ya Waziri Mkuu

Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa jana Jumapili Machi 26, 2023 na Ofisi ya Waziri Mkuu, wamiliki wa magari hayo wametakiwa kuyasajili Latra huku madereva nao wakitakiwa kutii na kufuata sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani kulinda usalama wa abiria na magari.

Madereva kudhibitiana

Mwenyekiti wa Madereva wa “Michomoko” Mkoa wa Simiyu, Mussa Stephano amesema chama hicho kimejiwekea mikakati ya kuwadhibiti madereva wote watakaobainika kukiuka sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani.

“Tutashirikiana na vyombo na mamlaka husika kuwadhibiti madereva wanaokiuka sheria na kanuni za usalama barabarani kuepuka ajali zinazoweza kuzuilika. Tumejifunza kupitia zuio lililopita, tutafanya kila lililo ndani ya uwezo wetu kufanya kazi zetu kwa kuzingatia sheria na kanuni zote za usafirishaji abiria,” amesisitiza Mussa

Kupitia mikakati hiyo, Umoja wa madereva hao umepanga kudhibiti tabia ya baadhi ya madereva kubeba abiria zaidi ya uwezo wa gari na kwenda mwendo kasi.