Wadukuzi wavamia mitandao taasisi za Serikali

Dar es Salaam. Wimbi la mashambulizi ya mitandaoni sasa limefikia taasisi muhimu za Serikali, baada ya wadukuzi kuteka akaunti rasmi ya YouTube ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Jeshi la Polisi Tanzania kwenye mtandao wa X (zamani Twitter) na kuweka taarifa potofu.
Taasisi hizo kwa nyakati tofauti zimetoa taarifa kujitenga na taarifa potofu zilizochapishwa na kueleza juhudi zinazofanyika kurejesha hewani akaunti zake rasmi.
Katika taarifa kwa umma, Jeshi la Polisi limesema taarifa zilizochapishwa kwa ukurasa wake hazikutoka katika vyanzo vyake rasmi.
“Jeshi la Polisi Tanzania linapenda kuuarifu umma kuwa kuna taarifa za uongo, zisizo na maadili na za upotoshaji zinazozunguka kwenye mitandao ya kijamii zikidai kutolewa na Jeshi kupitia akaunti yake ya X,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeeleza: “Taarifa hizo si za kweli na ieleweke kuwa Jeshi la Polisi haliandai wala kusambaza taarifa za aina hiyo kupitia mitandao yake ya kijamii.”
Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa uchunguzi umeanzishwa ili kuwabaini na kuwatia mbaroni wote waliopanga na kusambaza ujumbe huo wa uongo.
Mamlaka zimeonya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kuhusika katika uundaji au usambazaji wa taarifa hizo.
“Tunatoa wito kwa umma kupuuza taarifa hizo na kuepuka kuzisambaza zaidi ili kuepuka madhara ya kisheria,” Jeshi la Polisi limesisitiza.
Hata hivyo, baada ya muda mamlaka hizo zimefanikiwa kurejesha udhibiti wa akaunti zote zilizoathiriwa.
Kufuatia matukio hayo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetoa onyo kwa wahusika, ikisema wana lengo la kuchochea taharuki na kuwatia hofu wananchi.
“Imebainika kuwa kuna wahalifu wanaofungua akaunti za mitandao ya kijamii kwa kutumia majina yanayofanana na taasisi rasmi za Serikali ili kuchapisha taarifa za uongo na za uchochezi,” alisema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa.
Wizara hiyo iliwakumbusha wananchi kutumia mitandao ya kijamii kwa uangalifu na kuthibitisha taarifa zozote zinazotia shaka kupitia vyanzo rasmi.
Aidha, ilibainisha kuwa Serikali tayari imeanza kuchukua hatua za kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika wote.
“Serikali inatoa onyo kali kwa watu wote wanaojihusisha na vitendo hivi vya uhalifu mtandaoni,” alisema Msigwa na kuwataka wananchi kufuatilia taarifa sahihi kupitia kurasa rasmi za Serikali kwenye Instagram, X na Facebook.