Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wafanyabiashara wa ng’ombe walia na ushuru machinjioni

Baadhi ya wafanyabiashara wa machinjio ya Vingunguti wakiwa wamesimama katika machinjio hayo. Picha na Pamela Chilongola

Muktasari:

  • Ng’ombe waliotakiwa kuchinjwa machinjio ya Vingunguti usiku kuamkia Julai 19, 2024 walikuwa 600, lakini ng’ombe 200 wamezuiliwa kuchinjwa hadi walipe ushuru wa Sh7,500 kila mmoja, jambo linalopingwa na wafanyabiashara.

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa Machinjio ya Vingunguti wamemwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati ongezeko la ushuru wa mnada wa usafirishaji na ukaguzi wa afya ya mifugo kutoka Sh7,500 kwa ng'ombe mmoja hadi Sh15,000 wakisema ni hasara kwa biashara yao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo Ijumaa Julai 19, 2024 wamesema ngombe zaidi ya 200 wamezuiwa kuchinjwa katika machinjio hayo wakidaiwa watoe ushuru wa mnada huo kwa kila mmoja Sh7,500 wakati walishalipia kwenye minada ya awali.

Mwenyekiti wa wafanyabiashra wa machinjio hayo, Emmanuel Siliyake amesema wakinunua ng’ombe kwenye minada ya awali wanalipa ushuru wa Sh7,500 kwa kila ng'ombe, lakini wanapofika katika machinjio hayo wanalazimishwa watoe tena kiasi cha Sh7,500 kwa ajili ya ushuru wa mnada.

"Mfanyabiashara anayenunua ng’ombe kwenye mnada wowote wa awali atalipia ushuru kwa ajili ya usafirishaji na ukaguzi wa afya ya mifugo Sh7,500 na nikimchukua ng'ombe huyu na kumpeleka  kwenye machinjio ya Vingunguti naambiwa tena nilipe Sh7,500.

“Wakati huo huo tunatakiwa tulipe ushuru wa Manispaa kwa ajili ya uchinjaji Sh11,000. Hii inatuumiza," amesema Siliyake.

Siliyake amesema kutochinjwa kwa ng’ombe hao kunawasababishia hasara na kushindwa kulipa mikopo waliyochukua benki kama mitaji ya biashara hiyo.

Mwenyekiti huyo alitoa mfano mfanyabiashara anaponunua ng'ombe kwenye mnada wa Ruvu anaruhusiwa kuwapeleka kwenye machinjio hayo kwa sababu wapo madaktari wanakagua, hivyo wanatakiwa kutoa Sh11, 000 kwa ng'ombe mmoja anayechinjwa.

"Ng’ombe waliozuiwa wasichinjwe wameshalipiwa kila mmoja Sh11, 000 kwa ajili ya uchinjaji, kwa nini wanatulazimisha tulipwe ushuru wa mnada mara mbili, huku meneja wa machinjio yupo chini ya halmashauri anawezaje kuzuia kuchinja wakati hatudai chochote.

"Mwenye mamlaka ya kuzuia kuchinja ni wizara husika na si meneja ametusababishia hasara kubwa kwa wafanyabiashara," amesema Siliyake.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Gabriel Makuya amesema ana mtaji wa Sh4 milioni ambapo ananunua ngombe watano na malipo anayolipia serikalini ni Sh130,000 kwa siku.

"Hivi kweli kuna kuendelea kwa mwezi unatoa kodi ya Sh3.9 milioni na mtaji wangu huu nimechukua mkopo benki, chupuchupu nyumba yangu kuuzwa wa sababu hela yote inaenda serikalini," amesema Makuya.

Akijibu malalamiko hayo, meneja wa machinjio hayo, Dk James Kawamala amesema jana usiku alipokea malalamiko ya wafanyabiashara hao wanaosema walinunua kwenye minada mingine, akiwataka wapeleke malalamiko yao ngazi nyingine za Serikali.

Amesema wameweka utaratibu ng'ombe wanapotoka mikoani ni lazima waingie kwenye mnada wa Pugu, ili wanunuliwe ndipo wapelekwe machinjioni.

"Serikali imeweka utaratibu kama mtu hajalipa ushuru wa mnada wa Pugu kwa ajili ya usafirishaji na ukaguzi wa afya ya mifugo anatakiwa alipie Sh7,500.

“Ndiyo maana tumeweka mtu kwenye machinjio ya Vingunguti, ili kuwakagua wafanyabiashara wasiopitia Pugu mnadani, lengo tumewapunguzia safari ya kulipa mara mbili," amesema Dk Kawamala.

Hata hivyo, wafanyabiashara hao baada ya kukaa kikao hicho waliruhusiwa kuchinja ngombe hao na Mkuu wa Idara ya Mifugo Manispaa ya Ilala bila ya kutoa ushuru huo waliokuwa wanatakiwa kutoa.