Wagonjwa 90, 000 wahitaji huduma za kibingwa

Muktasari:
Zaidi ya wagonjwa 210,000 wamepata huduma ya matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Nkinga huku wagonjwa zaidi ya 90,000 wakihitaji huduma za kibingwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Tabora. Zaidi ya wagonjwa 210,000 wamepata huduma ya matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Nkinga huku wagonjwa zaidi ya 90,000 wakihitaji huduma za kibingwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Akizungumza katika uzinduzi wa Nkinga Polyclinic mjini Tabora Septemba 6, 2023 Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Tito Chaula amesema wastani wa wagonjwa 70,000 wamekuwa wakitibiwa kwa mwaka huku wastani wa wagonjwa 30,000 wakihitaji huduma za madaktari bingwa na madaktari bobezi.
“Tumeona uhitaji wa watu katika huduma za kibingwa kwa akinamama, watoto na magonjwa ya ndani,”amesema
Dk Chaula ameeleza katika Nkinga Polyclinic wamehudumia zaidi ya waginjwa 500 kwa muda wa siku nne na kuwa wanatarajia kuhudumia zaidi ya wagonjwa 900 hadi jumamosi watakapomaliza utoaji wa huduma bure ambapo watafanya hivyo mara mbili kila mwaka.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Nkinga ambayo inamilikiwa na kanisa la FPCT, Victor Nkungwe amesema wamefungua kituo hicho kwa lengo la kuwapunguzia muda na umbali wagonjwa wanaohitaji huduma za kibingwa sanjali na kuwasogezea huduma hizo mjini Tabora.
Amesema wanatanua wigo wa utoaji huduma kwa wagonjwa ambao watahudumiwa na wafanyakazi wenye weledi mkubwa,unyenyekevu na hofu ya Mungu kama ilivyo kawaida yao katika huduma zinazotolewa na kanisa la FPCT.
Akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Zakaria Mwansasu amepongeza uamuzi wa kuwa na kituo mjini Tabora na kuwa Serikali itatoa ushirikiano wakati wote.
Amewataka kuendelea kutoa huduma kwa weledi na kufuata miiko ya taaluma yao kwani wanafanya kazi ya Mungu ya Kuponya na kuisaidia Serikali katika eneo la utoaji huduma na matibabu ili wananchi wawe na afya njema na kutoa mchango wao kwa Taifa.
“Nimefanyiwa upasuaji wa jicho jana na leo naendelea vizuri na hali yangu naiona nzuri,”amesema Mwanaid Zubery aliyekuwa akisumbuliwa na jicho
Naye Juma Shaban amesema amepata huduma nzuri baada ya kupima shinikizo la damu, kisukari, figo na macho akigundulika na tatizo la macho ambalo amepatiwa miwani kwa gharama ndogo.