Wahitimu NIT washauriwa kutumia ubunifu kutengeneza ajira

Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC,) Abdi Mkeyenge
Muktasari:
- Wahitimu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) wameshauriwa kutumia ubunifu na maarifa waliyoyapata kutengeneza ajira sio kutegemea kuajiriwa pekee.
Dar es Salaam. Wahitimu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) wameshauriwa kutumia ubunifu na maarifa waliyoyapata kutengeneza ajira sio kutegemea kuajiriwa pekee.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam leo Jumamosi Desemba 4, 2021 na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Abdi Mkeyenge wakati wa maadhimisho ya Kongamano la nane la wahitimu wa chuo hicho hicho.
Katika kongamano hilo ilibainisha malengo yake ya ushindani katika kuwandaa wanafunzi wenye ujuzi na ubunifu watakaoweza kutengeneza ajira kupitia fursa ambazo Serikali imezitangaza ikiwemo uchumi wa Buluu, ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere na ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga Tanzania.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mkeyenge amesema wanapaswa kutumia ubunifu na maarifa wanayofundishwa chuoni hapo kwa manufaa ya jamii nzima.
“Tuache kabisa dhana ya kuajiriwa bali tufikilie zaidi kujiajiri, najua ujuzi, maarifa na tafiti mlizozipata hapa chuoni ni nyenzo kubwa kwetu katika kutengeneza jira, zinduka sasa na chukua hatua ya kujiajiri pale unapoona fursa ya kufanya hivyo,” amesema
Awali akizungumza katika Kongamano hilo Mkuu wa Chuo cha NIT, Profesa Zacharia Mganilwa amesema kongamano hilo limelenga kuwakutanisha walimu, wanafunzi na wahitimu kwa kuwaonesha dira baada ya kuhitimu na namna ya kutumia maarifa waliyoyapata kwa vitendo.