Wahitimu ualimu watakiwa kuzingatia maadili, weledi

Wahitimu wa mafunzo ya ualimu wakiwa katika mahafali yao katika Chuo cha Ualimu Tandala mkoani Njombe leo Aprili 13, 2024. Picha na Seif Jumanne

Muktasari:

  • Walimu mkoani Njombe wametakiwa kuacha kufundisha kwa mazoea badala yake wazingatie maadili na weledi wa kazi yao.

Njombe. Walimu wametakiwa kuacha kufundisha kwa mazoea na badala yake wazingatie maadili na weledi katika kazi zao ili kuleta matokeo chanya kwa wanafunzi wanaowafundisha.

Hayo yamesemwa leo Aprili 13, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, William Makufwe kwenye mahafali ya 46 walimu wa msingi na awali wa ngazi ya astashahada katika Chuo cha Ualimu Tandala kilichopo wilayani Makete.Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Makete, William Makufwe akizungumza katika mahafali ya ualimu katika Chuo cha Ualimu Tandala mkoani Njombe. Picha na Seif Jumanne

Amesema ipo changamoto kubwa ya walimu kufanya kazi ya kufundisha kwa mazoea na mwisho wa siku wanafunzi hawafanyi vizuri katika masomo yao.

Amesema wanafunzi walio wengi inapokuja mitihani wanafeli na hata wanaofaulu ni wachache na kwa kiwango ambacho hakiridhishi.

"Sasa nyinyi wahitimu wa leo mtakapopangiwa vituo vya kufanyia kazi naomba mkawe chachu ya mabadiliko kwenye shule mtakazopangiwa," amesema Makufwe.

Amewataka wahitimu hao kutanguliza nidhamu na kujituma na kuwa wa kwanza kukemea wanapoona jambo linaharibika ili wawe mabalozi wazuri wa chuo hicho.

Ameupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kuongoza kwenye mitihani yao ya kitaifa ya kuhitimu kwa takribani miaka mitatu mfululizo.

Awali Mkuu wa Chuo hicho, Vedasto Kibyala amesema chuo hicho kimeongoza kitaifa katika mitihani kwa miaka mitatu mfululizo kwa wanafunzi wake kufaulu kwa asilimia mia moja.

Amesema mwaka jana walikuwa na wanachuo 185 na kati yao 27 walipata alama ya juu kabisa za ufaulu na kupelekea kuongoza kitaifa katika mitihani hiyo.

"Chuo chetu kimejipambanua kuhakikisha kinawafundisha walimu bora, kuwaandaa na kuwasimamia ili kuhakikisha wanafundishwa kadiri mtaala unavyoelekeza," amesema Kibyala.

Mwenyekiti bodi ya chuo hicho, Jassery Mwamala amesema chuo hicho kinawaandaa walimu kuwa bora ili kuweza kulitumikia taifa lao.

"Pamoja na kuwa tunataka wakajitegemee, lakini nia ya sisi wazazi ni kuwa wawe na ajira, hivyo tulikuwa tunafikiri ni vizuri tunapopika vijana hawa na ajira ziwepo," amesema Mwamala.

Majaliwa Mungo, mmoja wa wahitimu wa kozi hiyo, amesema elimu waliyoipata watakwenda kuitumia kulingana na mazingira yatakayokuwepo ili kuinua kiwango cha elimu nchini.

"Walimu wengi wamezoea kufundisha kwa kuchukua kitabu na kwenda nacho darasani kufundisha, hawaangalii wahitaji waliopo darasani wanataka kutumia nini," amesema Mungo.