Wahitimu wa kada za afya wapewe neno
Baadhi ya wahitimu wa Chuo cha KCMUCo wakiwa wanakula kiapo cha maadili kabla ya kutunukiwa vyeti vyao. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Wahitimu wa kada mbalimbali za afya nchini wametakiwa kutoa huduma za afya zisizo na dosari kwa wagonjwa, huku wakizingatia misingi ya taaluma zao pamoja na kuwa na hofu ya Mungu katika utatibu wao.
Moshi. Wahitimu wa kada mbalimbali za afya katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Kikristo cha Tiba cha Kilimanjaro (KCMUCo), wametakiwa kutoa huduma za afya bila ubaguzi huku hofu ya Mungu ikiwaongoza na hivyo kutosababisha madhara wakati wa utoaji wa huduma.
Pamoja na kufuata misingi hiyo ya utoaji wa huduma za afya, wahitimu hao pia kujiamini katika kutenda wajibu kwa umahiri mkubwa.
Rai hiyo imetolewa leo Jumamaosi, Novemba 18, 2023 na Mkuu wa chuo hicho, Profesa Ephata Kaaya wakati wa mahafali ya 24 ya chuo hicho ambapo jumla ya wahitimu 451 kutoka kada mbalimbali za afya wamehitimu mafunzo yao.
"Ni mategemeo yetu sisi sote pamoja na taifa kwa ujumla kuwa ninyi mtakuwa msaada wa kuboresha afya za wale mtakaowahudumua katika jamii zetu, tumieni viapo vya taaluma zenu ikiwa ni dira ya kuwaongoza na kuzingatia taratibu za maadili ya taaluma zenu na huduma mtakazotoa kwa wagonjwa na jamii yote bila ubaguzi," amesema Profesa Kaaya na kuongeza;
"Kwa kuwa mfumo wa masomo yenu katika chuo kinachoamini uwepo wa Mungu na kwa kuwa kumcha Mungu ndio chanzo cha maarifa, basi matendo yenu mema kwa kjamii yamtukuze Mungu kwa kuonyesha upendo kwa wagonjwa na jamii yote popote mtakapokuwa mnatoa huduma za afya."
Amewataka wahitimu hao, wakawe mabalozi wazuri kutoka katika chuo hicho, kwa kuendelea kumcha Mungu na kutoa huduma zisizo na dosari kwa jamii na kuhakikisha huduma wanazozitoa wazinatoa kwa upendo kwa wagonjwa.
Naye Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Joseph Parsalaw, amewataka wahitimu hao wakawe madaktari wanaojiamini katika taaluma zao na kutenda wajibu wao kwa umahiri mkubwa huku wakimtanguliza Mungu katika kazi zao za utabibu.
"Daktari anapomhudumia mgonjwa akapona huna chakulipwa zaidi ya kusema nashukuru asante, ni jambo kubwa sana katika jamii, jamii ya watanzania inawaamini sana na inawategemea sana, wapendwa madaktari malipo yenu siku zote ni shukurani wala sio kitu kingine,” amesema na kuongeza;
“Shukrani hiyo ni kubwa kuliko chochote fanyeni kazi kwa bidii na uadilifu kwa kufanya hivyo mtatukuka katika utumishi wenu na Mungu atawakirimia mema."
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, Profesa Esther Mwaikambo amesema: “Nendeni mkatumie maarifa mliyoyapata mkaonyesha umahiri wenu katika kutoa pamoja na kuwa wafumbuzi wa mambo.”
Pamoja na mambo mengine, Profesa Mwaikambo, ameishukuru serikali kwa kuwafungulia programu 19 zilizokuwa zimefungiwa kudahili wanafunzi mwaka 2017/18 na kusema chuo hicho kimeweza kupata mafanikio makubwa na kwamba idadi ya wanfunzi imeongezeka na kufikia wanafunzi 2930.